Ticker

6/recent/ticker-posts

FURSA ZILIZOPO KWENYE MKONGE NI RAFIKI WA MAZINGIRA

Mkurugenzi mkuu TSB Saddy Kambona akisalimiana na Mkuu wa Kikosi cha KMKM Commodore Azana Msingiri.
Mkurugenzi mkuu TSB Saddy Kambona kushoto akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmahid Nsekela.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba katikati akisalimiana na mkuu wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) Commodore Azana Msingiri kulia, kushoto Mkurugenzi mkuu TSB Saddy Kambona.
Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Mkonge nchini Saddy Kambona akiongea na vyombo vya habari.


*************************

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

MKUU wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba amesema zao la Mkonge lina fursa nyingi katika uwekezaji wa fursa ya viwanda nchini ikiwamo uendelezaji viwanda vya kutengenezea vifungashio ambavyo ni rafiki kwa mazingira.


Mgumba ameyasema hayo katika semina kwa ajili ya wafanyabiashara, wajasiriamali na wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Tanga kuelezea fursa zipi zilizopo mkoani hapa na namna benki hiyo ilivyojipanga kuwasaidia ikiwamo mikopo kwa wakulima.


Alisema kwenye kilimo kuna mazao mbalimbali yanayolimwa kwa wingi mkoani hapa lakini inatambulika kuwa zao la Mkonge ni zao la kimkakati katika ukanda wa Kaskazini.


"Kwenye uendelezaji wa viwanda kuna uzalishaji wa magunia kwa ajili ya kubebea mazao ya kilimo, usokotaji wa kamba na uzalishaji wa mazuria, nafahamu Benki ya CRDB inatoa mikopo ya ununuzi wa mitambo ya kuchakata Mkonge (korona) na ununuzi wa zana bora za kilimo hususani matrekta kwa ajili ya kulima na kubeba Mkonge"


“Nawapongeza wadau wetu Benki ya CRDB muendelee kuongeza jitihada kutafuta suluhisho la fedha katika mnyororo wa thamani kwenye kilimo cha Mkonge kwa manufaa ya Watanzania wenzetu pia kwa Wanahisa wenu kwa kuongeza faida" amesema.


Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona pia ameipongeza CRDB kwa kuona umuhimu wa kuwakutanisha wadau na kuwapatia semina ya fursa mbalimbali walizo nazo ambazo zinachangia na kuchochea shughuli za maendeleo ikiwamo kilimo cha Mkonge.


“Bodi ya Mkonge tunapongeza hatua ya Benki ya CRDB kutupatia semina ya fursa mbalimbali walizo nazo, kwa sababu inasadia kuwafungua wakulima wetu na wadau mbalimbali kujua namna gani watafanikiwa katika hizo fursa kuhakikisha kwamba wanaongeza uzalishaji wa zao la Mkonge na kutumia fursa ambazo zinajitokeza katika Mkoa wa Tanga".


“Kama ambavyo sasa hivi tunaona Mkoa wa Tanga unafunguka, Bandari imepanuliwa, uwezo wa kuchukua mzigo mkubwa umeongezeka sana, kwa hiyo zile shehena za Mkonge zinazopitishwa katika bandari nyingine watambue kwamba sasa fursa imekuja karibu kupitisha mkonge na bidhaa nyingine zinazotokana na Mkonge,” amesema Kambona.


Aidha Kambona alisema Bodi ya Mkonge itahakikisha inaongeza uzalishaji na kutumia hiyo fursa vizuri zaidi katika kuongeza pato la Mkoa wa Tanga.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema semina hiyo iliyoandaliwa mahususi kwa ajili ya wafanyabiashara, wajasiriamali na wadau wa CRDB Mkoa wa Tanga itawawezeaha kutambua fursa zilizopo kwenye mkoa huo na benki hiyo imejipanga vipi kuwasaidia.

Post a Comment

0 Comments