Ticker

6/recent/ticker-posts

MAFUNZO KAZINI KWA WALIMU WA SOMO LA HISABATI SHULE ZA MSINGI YAMEFUNGULIWA RASMI


**********************

Mafunzo kazini kwa walimu wa shule za Msingi wa Somo la Hisabati yamefunguliwa rasmi leo tarehe 04/11/2022 ambayo yamefanyika kwa njia ya mtandao.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu, Bwana Venance Manori ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Msingi Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia amesema, mafunzo hayo yenye lengo la kuwawezesha walimu wa Elimu ya Msingi katika kufundisha na kujifunza Somo la Hisabati, ambayo yanafadhiliwa na World Bank kwa kuwezeshwa na Wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Shanghai-Normal na Taasisi ya Elimu Tanzania.

Bwana Manori amesema kuwa, mfumo wa Elimu wa Shanghai ni bora zaidi duniani hivyo Tanzania imepata bahati ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu ufundishaji na ujifunzaji wa Somo la Hisabati.

"Nina imani washiriki wa mafunzo haya watashiriki kikamilifu katika kupata maarifa na ujuzi kuhusu mbinu za kufundisha na kujifunza mada mbalimbali za Somo la Hisabati kama Algebra, Measurement, Integers, Geometry, Numbers na Statistics" amesema Manori.

Aidha, Manori amesema kuwa, washiriki wa mafunzo haya watapata muda wa kufanya majaribio ya vitabu vya Somo la Hisabati vya Darasa la I hadi III vilivyoandaliwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Shanghai-Normal.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt. Aneth Komba amesema kuwa kwa sasa mafunzo haya yanafanyika katika shule za Msingi za Serikali zinazotumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia na kujifunzia ambazo ni Shule ya Msingi Chang'ombe iliyopo Jijini Dar es Salaam na shule ya Msingi Azimio iliyopo Jijini Mbeya.

Dkt. Komba amewataka walimu watakaopatiwa mafunzo haya wakawasaidie walimu wengine kupata ujuzi watakaoupata kwa njia mbalimbali ili kuweza kukabiliana na changamoto za ufundishaji na ujifunzaji wa Somo la Hisabati.

Aidha, amewashukuru wataalamu kutoka Chuo kikuu cha Shanghai na kuahidi kutoa ushirikiano katika kutekeleza mafunzo haya.

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka World Bank, Dkt. Xiaoyan Liang amesema kuwa mafunzo haya yanatarajiwa kutolewa kwa walimu zaidi ya 17 kutoka katika shule za msingi za serikali zilizo katika mpango huu wa awali.

Dkt. Liang ameongeza kuwa, walimu wa Tanzania wana mengi ya kujifunza na kubadilishana uzoefu na wenzao wa Shanghai kwa kuwa Shanghai imekuwa na mafanikio makubwa katika ufundishaji na ujifunzaji wa Somo la Hisabati.

Post a Comment

0 Comments