Ticker

6/recent/ticker-posts

OFISA MISITU WILAYA NA WATENDAJI WAKAMATWA, WANANCHI 27 WASAKWA UBADHIRIFU MALI YA UMMA



*********************

Na Hamida Kamchalla, HANDENI.


WATUMISHI na viongozi wa Serikali ya Wilaya ya Handeni wapatao wanne wamekamatwa na kuwekwa ndani, huku wananchi 27 wakitafutwa na TAKUKURU kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali za umma wilayani humo.


Agizo la kukamatwa kwa viongozi hao limetolewa na mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kwamsisi wakati alipokwenda kusikiliza kero za wananchi ambapo alisema waliotumia vibaya madaraka yao.


Kufuatia hali hiyo na maelezo ya wananchi, Mgumba aliwasimamisha viongozi wa vijiji kutoa maelezo yao, ambapo Mgumba alibainisha kwamba,


"Kuna rushwa hapa inaonekana inaendelea, haiwezekani kukawa Kuna watu wanachukua mali za umma kwa maslahi yao binafsi halafu tunakaa tunabembelezana, viongozi wa vijiji wasimamie watoe maelezo yao" amesema.


Aidha baada ya viongozi hao kutokuwa na majibu ya kuridhisha huku wakiwataja baadhi ya wananchi na watendaji wa serikali vijijini humo, mkuu huyo alitoa maagizo kwa TAKUKURU na kusema,


"TAKUKURU kamata hawa viongozi na watendaji pamoja na hao wananchi 27 waliowataja hapa wakidai ardhi hiyo ni yao watafuteni wote peleka ndani, kama kuna serikali mliokua mnajaribu kuitania siyo hii" amebainisha.


Pia Mgumba amesisitiza kwamba, lengo la kutembelea wananchi hao ni kusikiliza na kutatua kero zao na kuwataka wazitoe kwa ushahidi ili serikali izipatie ufumbuzi au hatua zitakazostahili.


"Niwahakikishie kwamba, kama kuna ardhi yoyote imeporwa kwa njia haramu ya kutengeneza, itarudi kwenye kijiji husika" alifafanua Mgumba.


Viongozi waliokamatwa ni mtendaji wa kijiji cha Kwamsisi Erick Chipindula, mwenyekiti wa kijiji cha Kwedikabu Rajabu Makamba, mtendaji wa kijiji hicho Zahara Sempule na Ofisa misitu Wilaya ya Handeni Elinihaki Mdee.


Viongozi wa vijiji hivyo wanatuhumiwa kwa nyakati tofauti kuuza maeneo yenye ekari kuanzia 500 pamoja na mbao zipatazo 1000.

Post a Comment

0 Comments