Ticker

6/recent/ticker-posts

ASILIMIA 48 TU KATI YA 100 WATOTO WA SHULE ZA AWALI WAANDIKISHWA JIJI LA TANGA.***********************

Na Hamida Kamchalla, TANGA.


MEYA wa jiji la Tanga Abdulrahman Shiloow amesema kiwango cha uandikishaji watoto wa shule za awali hakijakidhi malengo kutokana na idadi ndogo ya walioandikishwa ambayo haijafikia kwenye asilimia 50, katika jiji hilo.


Shiloow ameyasema hayo ofisini kwake mbele ya waandishi wa habari, kwamba malengo ya jiji waliyojiwekea katika kuandikisha watoto wa shule hizo ni asilimia 100 lakini hadi sasa idadi hiyo haijafikiwa hata nusu yake jambo linaloashiria kuwa watoto wengi hawajaandikishwa.


"Tumefanya tathimini kwa uandikishaji watoto shule za awali na mpaka sasa imeonesha tumeandikisha watoto kwa asilimia 48 tu kati ya 100, tulitegemea tuandikishe watoto zaidi ya 6400, lakini mpaka sasa hivi tumeandikisha watoto 3200, maana yake kuna watoto zaidi ya 3200 hawajaandikishwa".


"Hivyo basi, tunawaomba na kuwasisitiza wazazi na walezi wa watoto wote, hata awe mlemavu naye ana haki, kwenda kuwaandikisha ili kutimiza malengo yetu katika jiji tuliyojiwekea" amesisitiza Shiloow.


Shiloow amefafanua kwamba halmashauri pia ilijiwekea malengo ya kuandikisha watoto zaidi ya 9300 lakini mpaka sasa wameandikisha watoto 5800 ambayo ni sawa na asilimia 62 huku zaidi ya asilimia 38 wakiwa hawajaandikishwa.


Aidha amebainisha kwamba, awali ilizoeleka watoto wanaanza kuandikisha kuanzia mwezi disemba hadi wa tatu, hali ambayo ilichelewesha watoto kuanza masomo yao, lakini kupitia tamko la serikali kazi ya uandikishaji imeanza na mpaka sasa walimu wapo shuleni wanaendelea na kazi hiyo ili inapofika mwezi wa kwanza watoto waanze masomo.


"Hivyo niendelee kuwasisitize na kuwaomba wazazi katika jiji hili na maeneo mengine kwamba uandikishaji wa watoto darasa la awali na la kwanza utamalizika rasmi disemba 30 mwaka huu, sasa niwaombe kwenda kuandikisha watoto ili wasiwakoseshe haki yao ya msingi kwani elimu ni bure" amesema.


Hata hivyo amesisitiza suala la lishe kwa watoto hao kwamba wazazi wazingatie milo ya watoto wao na kufuatia hilo waweze kuchangia chakula shuleni kupitia kamati zao kama wanavyoweza kuchangia madaftari na sare za shule, ili watoto hao wapate uelewa mzuri wanapokuea darasani.


"Elimu ili iwe bora ni lazima iendane na suala zima la lishe hususani kwa watoto wetu hawa wa madarasa ya awali, la kwanza, la pili na ltatu, watoto hawa hawana uwezo wa kuvumilia kushinda njaa, kwahiyo wazazi kupitia kamati zao za shule,


"Suala la lishe ni la kuchangia kwasababu linamgusa mtoto moja kwa moja, elmu bora inapatikana pale mtoto atakapokuwa ameshiba na kukaa vizuri darasani lakini pia itasaifia kumjengea uwezo wa kushika masomo vizuri kwa sababu mtoto bila lishe akili yake inadumaa" amesema.

Post a Comment

0 Comments