Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT. TAX: WANAWAKE KUJIAMINI, KUJITUMA NDIYO SIRI YA MAFANIKIO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) amewataka wanawake kujiamini, kujituma, kujiendeleza, kuwa waungwana na waadilifu wanapotekeleza majukumu yao kwani hiyo ndiyo siri ya mafanikio yao kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Dkt. Tax ametoa wito huo alipofungua programu ya mafunzo ya uongozi kwa viongozi wanawake Tanzania, yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi, Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Tax ameongeza kuwa wanawake wanapswa kuimarisha uwezo wao, kutumia weledi, busara na werevu wa kushawishi, kutiana moyo, kujadili kwa umakini na kufanya maamuzi kwa umahiri na kujiamini, ili nafasi ya mwanamke katika uongozi ithaminiwe na kuthibitisha kuwa watoto wa kike na wanawake wanao uwezo.

Aidha, Waziri Dkt. Tax amesema kuwa uwakilishi wa wanawake katika nafasi za uongozi na ngazi za maamuzi umekuwa ukikua kwa kasi ndogo duniani kote licha ya jitihada mbalimbali za kitaifa na kimataifa zinazoendelea.

Amesema Idadi ya wanawake viongozi katika taasisi za umma, asasi za kiraia na sekta binafsi imekuwa ikiongezeka ikilinganishwa na miongo iliyopita, lakini bado kasi ni ndogo.

“Tanzania imekuwa ya mfano katika suala hili kwani karibu kila sekta ina wanawake katika nafasi za uongozi na idadi imekuwa ikiongezeka. Tunao viongozi wanawake ambao wanatia hamasa kwa wanawake wanaochipukia katika masuala ya uongozi,” alisema Dkt. Tax

Waziri Tax amesema ripoti ya Umoja wa Mataifa na Chama cha Mabunge Duniani inaonyesha kuwa hadi Januari 2021, nchi za Bara la Ulaya zikiwemo Norway, Finland, Iceland na Denmark, zinaongoza kwa kuwa na idadi ya wanawake viongozi kwa zaidi ya asilimia 50 kwenye nyadhifa za uwaziri na watendaji wakuu serikalini huku idadi ya wanawake wanaosimamia Wizara nchini Marekani imeongezeka kutoka asilimia 17 mwaka 2020 hadi asilimia 46 mwaka 2021.

Kwa upande wa Tanzania, “takwimu zinaonesha kuwa tuna asilimia 26 ya wanawake viongozi. Idadi ya Mawaziri wanawake imeongezeka kutoka asilimia 21 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 35 mwaka 2022. Idadi ya Wakurugenzi wanawake imeongezeka kutoka asilimia 19 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 26 mwaka 2022. Idadi ya Majaji wanawake imeongezeka kutoka asilimia 39 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 40 mwaka 2022. Vilevile, idadi ya Wabunge Wanawake kwa mwaka 2022 ni asilimia 36.7 na walioteuliwa ni asilimia 57. Licha ya ongezeko hili, bado tuna kazi ya kuendelea kuwawezesha Wanawake katika sekta mbalimbali ili tuweze kufikia taifa lenye usawa wa kijinsia katika masuala ya Uongozi,” alieleza Waziri Tax .

Waziri Tax aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuandaa na kuboresha, sera, sheria, kanuni na miongozo ambayo ni rafiki na wezeshi kwa jinsia zote ili kuiwezesha jamii hususan mwanamke kukabiliana na changamoto.

Awali akiongea kabla ya ufunguzi wa mafunzo hayo, Balozi wa Finland nchini, Mhe. Theresa Zitting amesema kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Taasisi ya Uongozi kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya usawa.

“Taasisi ya uongozi bado ina jukumu la kufundisha zaidi watu wengi katika jamii za kitanzania hususan kuwajengea uwezo wanawake ili kuwawezesha kuondokana na unyanyasaji wa kijinsia, kuwapa nafasi ya kutoa maamuzi na kuwaweseha kutekeleza majukumu yao vyeme kwenye jamii zao,” alisema Balozi Theresa.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN – Women) nchini, Bi. Hodan Addou amesema mwanamke anahitaji msaada na mafunzo ya uongozi ili kumuimarisha na kumwezesha kufanya maamuzi sahihi katika jamii.

“Ni matumaini yangu kuwa kupitia mafunzo haya mtapata ujuzi ambao utawafanya kuwa viongozi bora katika jamii na kuwawezesha kufika malengo yenu kwa weledi zaidi ya sasa,” alisema Bi. Hodan


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akitoa hotuba ya ufunguzi wa programu ya mafunzo ya uongozi kwa viongozi wanawake Tanzania, yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi, Jijini Dar es Salaam
Balozi wa Finland nchini, Mhe. Theresa Zitting akielezea fursa na changamoto za uongozi kwa mwanamke katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa viongozi wanawake Tanzania, yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi, Jijini Dar es Salaam
Mwakilishi wa Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN – Women) nchini, Bi. Hodan Addou akielezea masuala ya wanawake katika mafunzo ya uongozi kwa viongozi wanawake Tanzania, yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi, Jijini Dar es Salaam
Meza kuu ikiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo ya uongozi kwa viongozi wanawake Tanzania, yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi, Jijini Dar es Salaam


Post a Comment

0 Comments