Ticker

6/recent/ticker-posts

HOSPITALI CHALINZE YAANZA HUDUMA ZA X-RAY


Mfamasia katika hospitali ya Wilaya ya Chalinze, akionyesha mtambo wa X-Ray unaotumika baada ya kupelekwa na MSD

Hospitali ya Wilaya ya Chalinze

*************************

Mwandishi Wetu

Pwani. Kuanza kutolewa kwa huduma ya picha za mionzi (X-Ray) katika Hospitali ya Wilaya ya Chalinze, kumewapunguzia wagonjwa adha ya kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 80 kufuata huduma hiyo.

Kabla ya huduma hizo katika hospitali hiyo, wagonjwa 15 hadi 20 walikuwa wanapewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Tumbi mkoani Pwani.

Hayo yameelezwa leo na Mfamasia wa hospitali hiyo, Shaaban Kinesi wakati akitoa taarifa ya uboreshwaji wa huduma za matibabu mbele ya Maofisa wa Bohari ya Dawa (MSD) walipotembelea hospitali hiyo.

Kutokana na umbali huo, amesema gharama na muda wa wagonjwa ulipotea zaidi ukilinganisha na hali ilivyo sasa.

"Hapo nyuma tulikuwa tunapata wagonjwa wa huduma za mionzi lakini tulikuwa tunawapa rufaa ya kwenda Tumbi ambapo kuna umbali wa kilometa 89.

"Hiyo ilikuwa inasababisha gharama na kupoteza muda mwingi kwa mgonjwa lakini MSD imetuletea huduma hizi zinapatikana katika hospitali ya Msoga," amesema.

Ameeleza kwa sasa katika hospitali hiyo kuna X-Ray mbili na zote zinatoa huduma, kadhalika wanayo majokofu kwa ajili ya chumba cha kuhifadhia maiti.

Mashine ya usingizi, vitanda na magodoro, amesema ni vifaa vingine walivyosambaziwa na MSD Katika hospitali hiyo.

Kuhusu upatikanaji wa dawa, Mfamasia huyo amesema kwa upande wao hali inaridhisha kwani dawa zote muhimu kutoka MSD zinapatikana kutokana na kuzingatia vigezo wakati wa maombi.

Kwa upande wake, Ofisa Huduma kwa Wateja Kanda ya Dar es Salaam, Mfamasia Diana Kimario amesema mahitaji yote muhimu yanaendelea kupelekwa kuhakikisha huduma bora zinaendelea kutolewa kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments