Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa zaidi ya shilingi bilioni saba kuwezesha ujenzi wa majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga ambacho awali kilikuwa kwenye majengo ya kanisa katoliki.
Akizungumza baada ya kuweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa majengo hayo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema fedha hizo zilikabidhiwa kwa wizara ya elimu ili isimamie ujenzi huo
Ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amendeleaa kutoa fedha za kuboresha miundombinu ya elimu katika ngazi zote ili kuwezesha upatikanaji wa elimu bora inayoendana na mahitaji ya nchi.
"Serikali imetafuta fedha ya kujenga majengo haya katika kata ya Pito ili kukabidhi majengo ya awali kwa kanisa katoriki, tunashukuru Manispaa ya Sumbawanga kwa kuweza kutoa eneo hili ili chuo kijengwe hapa" ameongeza Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Mkuu ameelekeza kufanyika uchunguzi wa Mhasibu wa chuo hicho pamoja na Katibu wa Kamati ya ujenzi wa mradi huo baada ya kukabiliwa na tuhuma za uchomaji moto nyaraka za ujenzi katika ofisi ya Mhasibu wa chuo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga amemweleza waziri Mkuu kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameridhia kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 100 kutumika kwa ajili ya kujenga majengo mapya ya vyuo vya ualimu.
Mhe. Kipanga amevitaja baadhi ya vyuo hivyo kuwa ni Chuo cha Ualimu Ndala, Kabanga, Shinyanga Dakawa, Muhonda na Sumbawanga ambavyo kuna vilivyokamilika huku vingine vikiendelea na ujenzi.
Kufuatia tuhuma za uchomaji moto ofisi ya Mhasibu chuoni hapo, Naibu Waziri amevunja kamati zote za ujenzi wa Chuo hicho na kuagiza kuundwa kwa kamati nyingine mara moja.
Ameongeza kuwa Serikali inamiliki vyuo 35 vya ualimu na kwamba vyuo 30 vimefanyiwa ukarabati mkubwa na kuongezewa miundombinu mipya ili kuhakikisha walimu wanatoa elimu bora katika mazingira bora.
Naye Mbunge wa Sumbawanga Mhe. Aesh Hilaly ameishukuru serikali kwa kujenga majengo hayo mapya ya chuo hicho, huku akiomba wasimamizi wa ujenzi kuhakikisha wanajenga majengo hayo kwa ubora.
0 Comments