Ticker

6/recent/ticker-posts

WAANDISHI WA HABARI TANGA WAFUNDWA MRADI WA SHULE BORA.



**********************

Na Hamida Kamchalla, TANGA.


TAKRIBANI sh bilioni 271 kutoka ufadhili wa Serikali ya Uingereza kupitia mfuko wa UK aid ikihusidha mradi wake wa Shule Bora zimelenga kuiunga mkono serikali katika kuinua kiwango cha elimu jumuishi nchini.


Mradi huo pia, umelenga kuweka mazingira salama ya kujifunzia kwa wanafunzi wote wa kike na wa kiume kuanzia shule za awali, msingi na mwanzo wa sekondari nchini.


Mratibu wa mradi wa shule bora Mkoa wa Tanga Thomas Aikaruwa amebainisha hayo katika mafunzo ya siku moja ya mradi wa shule bora kwa waandishi wa habari Mkoa wa Tanga na kusema kuwa mradi huo ni kuhakikisha kuwa elimu jumuishi inaboreka ambayo itatolewa kwa watoto wote.


"Kwa ushirikiano wa serikali yetu mradi huu utafanya maboresho yatakayowezeaha kila mtoto kupata msingi mzuri katika elimu yake ya awali, ili kutoa fursa kwa kutoa mchango wake katika ukuaji wa nchi na maendeleo yake" amesema.


Aidha Aikaruwa amesema mradi huo unafanya kazi katika mikoa 9 ambayo ni Dodoma, Katavi, Kigoma, Mara, Pwani, Rukwa, Simiyu, Singida na Tanga na makao yake makuu yakiwa Mkoa wa Dodoma.


"Mradi unalenga katika maeneo manne ambayo ni kujifunza kwa watoto wote shuleni, kufundisha ambapo mfuko wa msaada wa UK utaunga mkono na kuimarisha kazi ya ufundishaji",


"Jumuishi pamoja na kujenga mfumo ambao mfuko wa UK aids utaunga mkono serikali na kuimarisha ili kupata au kuwa na thamani ya fedha katika utoaji wa elimu katika ngazi zote kuanzia chini hadi Taifa" amesema.


Hata hivyo alisema jumuishi ni kipaumbele cha mradi huo ambao utawatupia macho kwa karibu wanafunzi wenye mahitaji maalumu na wale wanaotoka katika mazingira magumu na kuwawezesha kuwa shuleni katika mazingira bora na salama hadi kufikia elimu ya sekondari.


"Hii ni pamoja na kuwashirikisha wazazi na jumuiya katika kuboresha usalama wa shule na kuondoa migogoro, kuhakikisha walimu wanazungumzia mambo ya jinsia na upatikanaji wa mahitaji ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu",


"Pia kutayarisha mazingira salama na kuwaunga mkono wasichana kushiriki pamoja na kujadili mambo yanayowahusu, lakini pia kuwasaidia katika kipindi cha hedhi" amebainisha Aikaruwa.


Kwa upande wake Mwenyekiti Msaidizi wa Tanga Press Club ambaye pia ni mwandishi wa habari Mwandamizi wa gazeti la mwananchi Burhani Yakubu ametoa shukurani kwa waandaaji wa mafunzo hayo ambayo yataleta tija kwa waandishi katika kuendelea kuuhabarisha umma.


Yakubu amesema kwa uzoefu uliopo kwa waandishi katika kuandika habari za elimu, imeonekana Tanga kuingia kwenye mradi huo ni tofauti ya matokeo ya darasa la saba.


"Tatizo ni kwamba wananchi wengi wanaona shule siyo zao kwamba shule ni ya mwalimu na mwenyekiti wa kijiji, na hii inatokana na kukosekana kwa uwazi na ushirikishwaji, unaweza ukakuta hata hizo fedha zinzoletwa kutoka serikalini hawapati taarifa na ndiomaana wanaona hakuna umuhimu wa kuchangia hata chakula shuleni".


Mafunzo ya shule bora yalitolewa kwa waandishi wa habari takribani 30 na Maofisa habari wa halmashauri za Wilaya 9 pamoja na Ofisa habari wa Mkoa yalifanyika katika halmashauri ya mji wa Korogwe chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Post a Comment

0 Comments