Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT. MOLLEL AONGOZA KIKAO KAZI CHA MABORESHO YA RUFAA KATIKA VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA.


**********

Na WAF- DSM.

NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameongoza kikao kazi cha kuboresha huduma za Rufaa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini ili kuondoa changamoto zinazoweza kuzuilika ikiwemo vifo.

Kikao hicho chenye lengo la kuboresha huduma kimefanyika leo Januari 5, 2023 Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Tiba, Wakurugenzi wa Hospitali za Taifa, Waganga Wakuu wa Wilaya na Wafawidhi katika hospitali za Wilaya.

Katika kikao hicho, wamejadili mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo hasa changamoto zinazojitokeza katika mfumo mzima wa Rufaa kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine.

Akiongoza kikao hicho Dkt. Mollel amesema, Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametekeleza wajibu wake wa kuboresha miundombinu na kuleta dawa na vifaa tiba, hivyo kuwataka viongozi katika Sekta ya afya kuimarisha ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Ameongeza kwa kuwatia moyo Wataalamu wa afya kufanya kazi kwa juhudi na kufuata miongozo na maadili ya utendaji kazi ili kuondokana na malalamiko kutoka kwa wananchi yanayoweza kuzuilika.

Aidha, Dkt. Mollel ametoa wito kwa Hospitali za juu kusidia hospitali za ngazi ya chini kwa kuzijengea uwezo kupitia njia ya mkoba, na kuwataka viongozi kujenga tabia ya kujinyenyekeza katika maeneo yao ya utendaji.

Nae Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Nagu amesisitiza juu ya ushirikiano na kusaidiana baina ya hospitali moja na nyingine ili kuongeza ufanisi katika utendaji na kuleta matokeo chanya ya huduma bora kwa wananchi.

Ameendelea kusema kuwa, kila hospitali iliyokatika ngazi ya juu ya utoaji huduma kwa wananchi ni lazima isaidie hospitali za ngazi ya chini kwa kuzijengea uwezo ili ziweze kuwasaidia wananchi kupata huduma bora zaidi.

Kwa upande wake Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Mariam Kisangi amesema kama Mwakilishi wa Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam anapongeza juhudi zinazofanywa na vituo vyote vya kutolea huduma na wanaendelea kuisimamia Serikali ili kuongeza jitihada katika kuboresha huduma nchini.

Nae, Mkurugenzi wa huduma za tiba Wizara ya Afya Prof. Paschal Ruggajo amebainisha mikakati mizuri iliyowekwa na Wizara ya Afya ikiwemo namna bora ya kushirikiana baina ya kituo kimoja cha kutolea huduma kwenda kituo kingine ili mgonjwa apate huduma bora bila usumbufu wowote.

Post a Comment

0 Comments