Ticker

6/recent/ticker-posts

MWILI WA JAJI DKT. UTAMWA KUZIKWA JUMAMOSI

Na Mary Gwera, Mahakama

Mwili wa aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Iringa, Mhe. Dkt. John Utamwa unatarajiwa kuzikwa Siku ya Jumamosi, tarehe 07 Januari, 2023 katika Kijiji cha Msemembo kilichopo Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo tarehe 03 Januari mwaka huu kutoka kwa Kaka wa marehemu, Dkt. Ashery Utamwa, mwili wa marehemu unatarajiwa kutolewa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) siku ya Jumatano jioni ya tarehe 04 Januari, mwaka huu na kupelekwa nyumbani kwake Madale-Tegeta jijini Dar es Salaam ambapo kutakuwa na ibada siku hiyo hiyo itakayofanyika kati ya saa 12 jioni na saa 1 usiku.

Aidha, Siku ya Alhamis tarehe 05 Januari mwaka huu, saa 7 mchana kutakuwa na ibada ya kuaga mwili wa marehemu itakayofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Albano lililopo Posta Mpya jijini Dar es Salaam.

Dkt. Utamwa ameeleza kuwa, mara baada ya ibada ya kuuaga mwili wa marehemu Jaji Dkt. Utamwa, mwili huo utapelekwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Dar es Salaam (JNIA) kwa ajili ya kusafirishwa Ijumaa asubuhi tarehe 06 Januari, 2023 kuelekea Dodoma na baadae utasafirishwa kwenda Kijiji cha Msemembo ambapo shughuli za maziko yake zitafanyika.

Marehemu Jaji Dkt. Utamwa alizaliwa tarehe mosi Julai, 1963 na alifariki dunia tarehe 02 Januari, 2023 akiwa katika Hospitali ya MNH alipokuwa akipatiwa matibabu. Marehemu amekuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la Damu ambapo tarehe 17 Desemba, 2022 alilazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa. Mnamo tarehe 18 Desemba, 2022 alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kuendelea kupatiwa matibabu hadi mauti yalipomfika.

Marehemu Jaji Dkt. Utamwa alijiunga na Mahakama ya Tanzania tarehe 17 Februari, 1992 akianzia ngazi Hakimu Mkazi. Alipanda ngazi mbali mbali ndani ya Mahakama na hatimaye aliteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania tarehe 24 Juni, 2010. Akiwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Marehemu Jaji Dkt. Utamwa alifanya kazi katika kanda za Dar es Salaam, Tabora, Mbeya na Iringa.

Kwa mawasiliano zaidi kuhusu taarifa zaidi za msiba huu, wasiliana na simu nambari 0747 452 269.
Marehemu Jaji Dkt. Utamwa enzi za uhai wake.

Post a Comment

0 Comments