Ticker

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA APONGEZWA KURUHUSU MIKUTANO YA HADHARA

Mwenyekiti akiongea na waandishi wa habari Mkoa wa Tanga.
Mwenyekiti wa UWT Taifa Mary Chatanda akisalimiana na wajumbe wa UWT Mkoa wa Tanga alipowasili katika ofisi za Ccm Mkoa.


************************


Na Hamida Kamchalla, TANGA.


UMOJA wa Wanawake wa Tanzania (UWT) unaungana na wito wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa wanasiasa kutumia ruksa ya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kwa kufanya siasa za kistaarabu , kupevuka na zenye kujenga na kuacha matusi na kashfa.


Akiongea na waandishi wa habari katika ofisi ya Ccm Mkoa wa Tanga, mwenyekiti wa UWT Taifa Mary Chatanda amesema Rais ni mpenda haki na ndio maana maamuzi matatu yaliyochukuliwa na Rais Samia juzi kwa vyama vya siasa yataendelea kukuza amani ya nchi.


"Siasa, ni mwelekeo mpya wa nchi yetu katika kuihami demokrasia yetu, sisi tunasema hakika Mama Samia ni neema kutoka kwa Mungu, kilio chetu UWT siku zote ni kuona nchi yetu ikiwa na utulivu, amani na yenye haki baina ya wananchi wake na serikali yao" amesema Chatanda.


"Rais Samia amechonga palio, wajibu wetu sote wanasiasa na wananchi wote ni kulifuata kwa unyenyekevu, tusimkatishe tamaa, vijana, wakina mama hata wazee, sote tuwe wamoja tujenge nchi yetu, UWT inawasihi viongozi wanawake ndani ya vyama vya siasa,


"Kuonyesha mfano katika hili kwa kutanguliza ustaarabu , kuheshimiana , utu wakati wote wa mikutano hiyo ya hadhara na kamwe pasitokee viongozi wa vyama vya siasa kubeza na kutweza utu wa mwanamke au wa mtu mwingine katika mikutano hiyo".

Aidha amesema UWT inawahimiza viongozi wanawake wa vyama mbalimbali kuandaa mikutano mingi ya hadhara ili kuweza kupokea kero mbalimbali zinazowagusa wanawake kwa kuwa wanawake wote nchini wanakabiliwa na kero zinazofanana bila kujali itikadi zao.


Chatanda amebainisha kwamba katika mikutano hiyo wanaoendeleza hatua mahususi za kuchukua kwa serikali ili kumkomboa mwanamke kiuchumi , kijamii na kisiasa lakini pia alisema wamefurahishwa na uamuzi wa serikali ya awamu ya sita ya kuridhia mapendekezo ya kikosi kazi ya kufanya marekebisho ya sheria kadhaa ndani ya nchi kwa nia ya kuimarisha demokrasia zaidi ambayo yatahusisha wananchi .


"Tunaimani marekebisho hayo pia yatazingatia masuala ya usawa wa kijinsia katika kuongeza uwakilishi wa wanawake kwenye siasa na uongozi kuanzia kwenye vyama vya siasa kama ambavyo tunashuhudia namna Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan anavyojitahidi kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye uongozi ndani ya serikali yake na chama anachoongoza cha CCM" amesema.


Amesema kwa niaba ya wanawake wa Tanzania wanaunga mkono uamuzi wa kukwamua mchakato wa marekebisho ya Katiba ya Tanzani, hivyo wanahimiza amani na utulivu wakati wote wa kusubiri serikali kukamilisha taratibu zote za kuanza mchakato huo.


"Lakini pia tunaendelea kuwaomba Watanzania kuendelea kumuamini Mheshimiwa Rais na kumuunga mkono kwani ana dhamira njema ya kujenga Taifa linaloongea lugha moja ambalo kila mmoja anashiriki katika ujenzi wa Taifa lake" amebainisha.


Naye Mjumbe wa NEC Mkoa wa Tanga Mohamed Salim Ratco ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa kuwa na mipaka katika kutandaza sera zao wanapokuwa kwenye mikutano yao.


Matarajio yetu ni kuona tunakuwa na siasa za kistaarabu katika ngazi zote, zisiwe za kuchafuata wala kutukanana kwenye majukwaa" amesema Ratco.

Post a Comment

0 Comments