Ticker

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA ATOA BILIONI 60 KUJENGA BARABARA YA LAMI MBINGA

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 35 kutoka Amani makoro hadi Ruanda wilayani Mbinga ambayo serikiali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 60 kutekeleza mradi huo kwa miezi 18 chini ya Kampuni ya China Raiway Seventh Group
Mkuu wa Mkoa wa nRuvuma Kanali Laban Thomas akiwa kulia na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mheshimiwa Aziza Mangosongo wakizungumza mara baada ya kuangalia moja ya madaraja yanayojengwa katika mradi wa barabara ya Amanimakoro hadi Ruanda wilayani Mbinga.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kuhusiana na utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Amanimakoro hadi Ruanda wilayani Mbinga yenye urefu wa kilometa 35
sehemu ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya lami ya Amanimakoro hadi Ruanda yenye urefu wa kilometa 35 ambapo hadi sasa utekelezaji umefikia asilimia 24


*******************


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya shilingi bilioni 60 kujenga kilometa 35 za lami wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.

Akitoa taarifa ya ujenzi huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma,Mhandisi Ephatar Mlavi amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara ya lami ya Kitai hadi Lituhi yenye urefu wa kilometa 82.

Hata hivyo amesema kiasi cha fedha kilichotolewa na serikali kinahusisha ujenzi wa barabara ya lami kwa kipande cha kutoka Kijiji cha Amanimakoro hadi Kijiji cha Ruanda,barabara yenye urefu wa kilometa 35.

Ameutaja mradi huo kuwa ulianza kutekelezwa Juni 15,2022 ambao unatarajiwa kutekelezwa kwa miezi 18, hivyo kukamilika Desemba 2023 ambapo amemtaja Mkandarasi wa mradi huo kuwa ni kampuni ya China Railway Seventh Group.

Amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa kilometa 35 za barabara kwa kiwango cha lami,ujenzi wa madaraja manne,ujenzi wa makalaveti makubwa saba na ujenzi wa makalavati madogo 58 na kwamba hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 24 .Tayari serikali imetoa fedha za kujenga kilometa 40 kati ya 82 .

“Barabara hii ina umuhimu mkubwa katika usafirishaji wa makaa ya mawe kwa sababu eneo hili lina migodi mingi ya madini hayo hivyo barabara hii itasaidia usafirishaji wa makaa ya mawe Kwenda sehemu mbalimbali nchini ikiwemo bandari ya Mtwara’’,alisisitiza Mhandisi Mlavi.

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi wa barabara hiyo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Kanali Laban Thomas amempongeza Mkandarasi kwa kufanya kazi ndani ya mkataba ambapo amesisitiza kazi hiyo ikamilike mapema ili wananchi waanze kunufaika nayo.

Ameitaja barabara ya Kitai-Lituhi kuwa ni miongoni mwa barabara kubwa mkoani Ruvuma yenye urefu wa kilometa 82 ambayo inategemewa na Mkoa katika kukuza uchumi na kwamba inaunganisha wilaya za Mbinga na Nyasa ,pia inaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Njombe kupitia wilaya ya Ludewa.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuchukua uamuzi wa kizalendo wa kutekeleza mradi huo unaoufungua Mkoa wa Ruvuma kupitia barabara ya Kitai-Lituhi.

Post a Comment

0 Comments