Ticker

6/recent/ticker-posts

BARABARA ZA MZUNGUKO ZA AINA YAKE SULUHU YA MSONGAMANO WA MAGARI DODOMA – ROSEMARY SENYAMULE


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara za mzunguko katika Jiji la Dodoma Lot 1 kutoka Nala-Veyula-Mtumba-Ihumwa yenye urefu wa kilometa 52.3 ambao ujenzi wake umefikia asilimia 21.3 na unatarajia kukamilika Desemba 2024. Mradi huo unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 100.8. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akikagua maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato ambao ujenzi wake umefikia asilimia 11.7 na utakapokamilika utaruhusu ndege 13 kutua kwa wakati mmoja na utahudumia abiria Milioni 1.5 kwa kutumia mageti 8. Mhe. Senyamule amemtaka Mkandarasi wa ujenzi kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.

*****************************

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametoa rai kwa wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa miradi ya kimkakati katika jiji la Dodoma kuzingatia ubora na viwango katika kukamilisha miradi kwa wakati.

Mhe. Senyamule ameyasema hayo leo Februari 15, 2023 wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Msalato, barabara ya mzunguko LOT 1 inayotoka Nala-Veyula-Mtumba-Ihumwa yenye urefu wa kilometa 52.3 na LOT 2 yenye urefu wa Kilometa 60 inayotoka Dry pot Ihumwa, Ngo’ngo’na, Matumbulu, Bihawana – Nala.

“Mradi huu ni wa aina yake barani Afrika tunampongeza sana Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za kukamilisha ujenzi wa kilometa 112.3 km za barabara za mzunguko ndani ya Mkoa wa Dodoma” Amefafanua Mhe. Senyamule.

“Sisi tunataka miradi yetu ikamilike ndani ya muda, sote tunafahamu miradi hii muhimu inatakiwa kukamilika 2024 au mapema 2025 kama mkataba unavyoonyesha. Dhamira ya serikali ni kusogeza huduma kwa wananchi na kuhikisha utekelezaji wa miradi hii unanufaisha wananchi ikiwa ni pamoja na kuzingatia utoaji wa huduma kwa jamii (CSR) kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na miongozo iliyopo.

Hatutamani sana tunaanza vizuri tunafika mahali tunaanza kutoa sababu nyingi, changamoto zitatueni lakini zisipelekee kuongeza muda wa mradi kukamilika’’ Alisisitiza Mhe Senyamule.

Akiwa katika eneo la ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato unaojengwa na Mkandarasi kutoka China Mhe Senyamule amemtaka Mkandarasi huyo kuongeza kasi ya ujenzi wa jengo la abira ili liweze kukamilika kwa wakati na kwenda sambamba na ujenzi wa njia za kuruka na kutua ndege.

“Hii miradi inabidi iende sambamba, hatuwezi kukamilisha mradi mmoja nakuanza kuutumia maana yote inategemeana, hakuna mkwamo wowote fedha za ujenzi zipo, sisi tunahakikisha kazi inaendana na kasi, lazima wakandarasi wajue matamanio ya Serikali, fanyeni kazi usiku na mchana” Amesisitiza Mhe. Senyamule.

Mradi wa Ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato Lot 1 sehemu ya kwanza utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 165 na Lot 1 sehemu ya 2 utagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 199

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri ametoa rai kwa Mkandarasi huyo kuhakikisha anazingatia Mpango wa Usimamizi wa Mazingira ili miundombinu inayojengwa hususan madaraja yaweze kupitisha maji kikamilifu bila kuathiri wananchi na mazingira kwa upande wa pili.

Katika ziara ya siku moja ya kutembelea miradi ya kimkakati ndani ya Mkoa wa Dodoma, Mhe. Mkuu wa Mkoa alimbatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya.

Post a Comment

0 Comments