Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Catherine Bamwenzaki leo Februari 10, 2023akifungua mafunzo kwa maafisa wa Serikali waliopo katika mpaka wa Horohoro mkoani Tanga, kuhusu udhibiti wa uingizaji nchini wa gesi na vifaa vyenye gesi zinazomong’onyoa tabaka la ozoni.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Dustan Shimbo leo Februari 10, 2023 akiwasilisha mada kuhusu Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (Kanuni za Kudhibiti Kemikali Zinazoharibu Tabaka la Ozoni), 2022, wakati wa mafunzo kwa maafisa wa Serikali waliopo katika mpaka wa Horohoro mkoani Tanga, kuhusu udhibiti wa uingizaji nchini wa gesi na vifaa vyenye gesi zinazomong’onyoa tabaka la ozoni.
Mhandisi George Ngosso kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) leo Februari 10, 2023 akiwasilisha mada kuhusu Athari zitokanazo na Uharibifu wa Tabaka la Ozoni na Udhibiti wa uingizaji nchini wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal wakati wa wa mafunzo kwa maafisa wa Serikali waliopo katika mpaka wa Horohoro mkoani Tanga, kuhusu udhibiti wa uingizaji nchini wa gesi na vifaa vyenye gesi zinazomong’onyoa tabaka la ozoni.
Mhandisi Goodluck Lulagora kutoka Wakala wa Mafunzo ya Elimu ya Uvuvi Bagamoyo (FETA) akitoa mafunzo kwa maafisa wa Serikali walipoko mpaka wa Horohoro mkoani Tanga kuhusu Matumizi ya Mitambo ya Kutambua Gesi zinazoharibu Tabaka la Ozoni leo Februari 10, 2023.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Catherine Bamwenzaki akiwa katika picha ya pamoja na maafisa wa Serikali waliopo katika mpaka wa Horohoro mkoani Tanga wakati wa mafunzo kuhusu udhibiti wa uingizaji nchini wa gesi na vifaa vyenye gesi zinazomong’onyoa tabaka la ozone yanayofanyika kwa siku mbili mpakani hapo.
(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)
************************
Wasimamizi wa sheria mipakani wametakiwa kusimamia na kudhibiti gesi zinazochangia kumong’onyoa tabaka la ozoni pamoja na kuchangia ongezeko la kiwango cha joto duniani hivyo husababisha mabadiliko ya tabianchi.
Pia, wametakiwa kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi tabaka la ozoni ambalo kama likimong’onyoka huruhusu mionzi zaidi ya urujuani kufikia uso wa dunia ambayo huathiri afya ya binadamu na mazingira na kuhamasisha matumizi ya gesi mbadala ambazo ni rafiki kwa afya ya binadamu na mazingira
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Catherine Bamwenzaki ametoa wito huo leo Februari 10, 2023 wakati akifungua mafunzo kwa maafisa wa Serikali waliopo katika mpaka wa Horohoro mkoani Tanga, kuhusu udhibiti wa uingizaji nchini wa gesi na vifaa vyenye gesi zinazomong’onyoa tabaka la ozoni.
Amesema kemikali au gesi zinazotumika katika majokofu, viyoyozi, vifaa vya kuzimia moto, usafishaji chuma, utengenezaji magodoro, ufukizaji wa udongo katika vitalu vya tumbaku, kilimo cha maua na hifadhi ya nafaka katika maghala ambazo huingizwa nchini kupitia mipaka mbalimbali husababisha madhara yakiwemo saratani ya ngozi, upofu na athari kwa ukuaji wa mimea na viumbe hai wengine.
Hata hivyo, alisema kuwa mwanzoni mwa miaka ya 1970 wanasayansi walivumbua kwamba baadhi ya kemikali zinazotengenezwa na binadamu hujipenyeza angani na kumong'onyoa tabaka la ozoni na uchunguzi wa angahewa tangu miaka hiyo umethibitisha kwamba tabaka la ozoni limekuwa likimong'onyoka kwa kasi ya asilimia tano kila muongo.
Mkurugenzi msaidizi huyo alibainisha kuwa matokeo ya uvumbuzi huu yalisababisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) kufanya tathmini ya kisayansi mwaka 1976 kuchukua hatua kulinda tabaka hilo.
“Chini ya Programu ya Taifa, Serikali pia imeandaa na inatekeleza Mpango wa Kuondosha Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni Jamii ya Hydrochlorofluorocarbons (HCFCs) ifikapo mwaka 2030 na chini ya mpango huu mojawapo ya shughuli zinazotelekezwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa maafisa Forodha na wasimamizi wa Sheria nchini kuhusu utekelezaji wa Kanuni za Usimamizi wa Mazingira yaani Udhibiti wa Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni za mwaka 2022 na utekelezaji wa Mikataba ya Vienna na Montreal Nchini.
Jumla ya maafisa wa serikali 720 kutoka mamlaka mbalimbali za udhibiti wamepatiwa mafunzo.
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi wa Forodha Kituo cha Horohoro Bw. Odero Ryoba ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutoa mafunzo hayo akisema yataleta tija katika majukumu yao.
Ameahidi kutumia elimu aliyopata kwa kushirikiana na watumishi wenzake katika kituo hicho kufanya kazi bega kwa bega na wataalamu kutoka taasisi zingine za Serikali kuhakikisha udhibiti wa kutosha wa uingizaji kemikali unafanyika.
Bw. Odero pia ametoa wito kwa Serikali kuendelea kutoa mafunzo kwa maafisa katika vituo vyote nchini ya kutambua kemikali haribifu kwa tabaka la ozoni ili iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Katika mafunzo hayo washiriki wameelimishwa kuhusu Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (Kanuni za Kudhibiti Kemikali Zinazoharibu Tabaka la Ozoni), 2022, mada iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Dustan Shimbo, Sayansi ya Ozoni.
Mada nyingine ni athari zitokanazo na uharibifu wa tabaka la ozoni & Udhibiti wa uingizaji nchini wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal na Mhandisi George Ngosso kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Matumizi ya Mitambo ya Kutambua Gesi zinazoharibu Tabaka la Ozoni – Mhandisi Goodluck Lulagora – Wakala wa Mafunzo ya Elimu ya Uvuvi – Bagamoyo (FETA) na Bw. Said Mziwanda kutoka VETA, Chang’ombe.
0 Comments