Ticker

6/recent/ticker-posts

BODI YA MICHEZO YA KUBAHATISHA (GBT) YATOA ELIMU KWA WATENDAJI WA MKOA WA PWANI

NA MWANDISHI WETU, KIBAHA

MKUU wa Mkoa wa Pwani Alhaj Aboubakar Kunenge amehimiza ushirikiano baina ya Taasisi za Umma, Binafsi na watendaji kwenye Halmashauri ili kazi ya kuwatumikia wananchi iwe rahisi.

Ameyasema hayo wakati akifungua semina ya kujenga uelewa wa shughuli za taasisi mbalimbali za umma na binafsi ikiwemo Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) na watendaji kutoka Halmashauri za Mkoa wa Pwani Machi 30, 2023.

GBT ni taasisi ya Kiserikali ambayo iko chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ikisimamiwa na Msajili wa Hazina. (TR).

RC Kunenge alisema wataalamu lazima wajue viongozi wa kisiasa hawawezi kuwa na maamuzi mazuri kama wataalamu hawatafanya kazi ya kitaalamu inavyotakiwa.

“Lazima tuelewe, serikali ni moja, mlipaji ni mmoja, fedha inatoka fungu moja na inavyopatikana iwe ni Halmashauri au Bodi ya Michezo ya kubahatisha yote inaingia sehemu moja kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha au PST.” Alisema na kuongeza ….

Haiwezekani kwenye Halmashauri kukawa na watendaji kutoka kila taasisi ya serikali na kushauri ili utendaji wa taasisi hizo kwenye maeneo ambayo ni vigumu kwa watendaji wao kuwepo ili kuwatumikia wananchi ni vema kukawepo na makubaliano yatakayowezesha utendaji kazi ukawa rahisi bila ya vikwazo, alifafanua Alhaj Kunenge ambaye alifuatana na Wakuu wote wa wilaya za Mkoa huo.

“Kama tuna majukumu ambayo tunaweza kufanya kwa niaba ya wenzetu mnaweza kukasimu shughuli zenu na zikafanywa na watu wa Halmashauri, lazima tufanye kazi kwa kushirikiana kwani serikali ni moja.” Alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Bw. James Mbalwe alisema Bodi imefika Mkoani humo kwa lengo la kujitambulisha rasmi kwa watendaji wa Mkoa ili kuongeza ufahamu wa kamati, uwepo wa taasisi na kuongeza ufahamu juu ya usimamizi na uendeshaji wa michezo ya kubahatisha hapa nchini.

Pia kuimarisha ushirikiano katika usimamizi na udhibiti wa sekta na kuomba kamati ya Ulinz na Usalama ya Mkoa kushirikiana na GBT ili kudhibiti wavunjaji wa sheria ya michezo ya kubahatisha hapa mkoa wa Pwani, alisema Bw. Mbalwe.

Alisema wanaona umuhimu wa kutoa elimu mara kwa mara kwa vile GBT ni taasisi change iliyoanzishwa mwaka 2003

Alisema semina kama hizo zimekuwa na manufaa makubwa katika kurahisisha utendaji wa GBT na kutolea mfano Mkoa wa Kigoma ambako baada ya kutolewa elimu kama hiyo utendaji wa Michezo ya Kubahatisha Mkoani humo imekuwa rahisi.

“Kazi yetu ni udhibiti, kusimamia na kuratibu uendeshaji wa michezo ya kubahatisha nchini na ieleweke kuwa GBT haifanyi biashara na iko chini ya Wizara ya Fedha chini ya Msajili wa Hazina.” Alifafanua

Bw. Mbalwe alihimiza kuimarisha ushirikiano katika usimamizi wa sekta na kuiomba kamati ya usalama ya mkoa kuongeza ushirikiano zaidi katika kudhibiti wavunja sheria ya Michezo ya Kubahatisha.

“Nina sisitiza Michezo ya Kubahatisha ni Burudani na sio Ajira au njia ya kujitafutia kipato.” Alifafanua Bw. Mbalwe.

Kuanzishwa kwa GBT kumewezesha sekta ya michezo ya kubahatisha kuratibiwa vizuri zaidi na iweze kuchangia ipasavyo katika pato la taifa na wananchi wanaojishughulisha kwenye michezo hiyo wanalindwa ipasavyo.

“Sekta inakuwa kwa kasi na kwa sababu hiyo kunahitaji uratibu makini ili iendelee kukua katika namna ambayo utaratibu unaopasa bila kupoteza malengo ya msingi ya kuanzishwa kwake.” Alifafanua Bw. Mbalwe.


Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Alhaj Aboubakar Kunenge akifungua semina hiyo kwenye Mji wa Kibaha Machi 30, 2023
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), Bw. James Mbalwe akizunguzma kwenye semina hiyo.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Pwani
Baadhi ya Wakuu wa Wilaya na watendaji wengine kutoka Halmashauri za Mkoa huo
Mkurugenzi Mkuu wa GBT, Bw. James Mbalwe (wakwanza kulia), Mkurugenzi wa Huduma za (DCS) Bw. Daniel Ole Sumayan (katikati) na Mkurugenzi wa Ukaguzi na Matekelezo Bw. Sadick Elimsu
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Alhaj Aboubakar Kunenge (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa GBT, Bw. James Mbalwe (wapili kushoto) Mkurugenzi wa Masuala ya Shirika, Bw. Daniel Ole Sumayan (wakwanza kushoto). Katikati ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Bw. Rashid Mchatta.

Picha ya pamoja

Post a Comment

0 Comments