Ticker

6/recent/ticker-posts

TUTUMIE FURSA YA GESI YA KUWEKEZA ILI KUWAFIKIA WANANCHI WENGI- BENOITE

Mwenyekiti wa Shirikisho la Kampuni za gesi Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas Araman Benoite akijadiliana jambo na baadhi ya wadau baada ya kumaliza kuzungumza katika Kongamano la Kimataifa la Shirikisho la Kampuni za gesi Afrika Mashariki linaloendelea nchini Tanzania
Mwenyekiti wa Shirikisho la Kampuni za gesi Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas Araman Benoite akitoa hotuba kwa niaba ya kampuni hizo leo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Shirikisho hilo Afrika Mashariki ambalo litafanyika kwa siku mbili nchini Tanzania

Wadau wa Kampuni za Gesi Afrika Mashariki na mataifa mengine duniani wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kufunguliwa kwa Kongamano la Kimataifa la Shirikisho la Kampuni za Gesi Afrika Mashariki ambalo litafanyika kwa siku mbili katika Jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania ambapo washiriki 800 wameshiriki.

Matukio mbalimbali katika picha wakati wa Kongamano la Kimataifa la Shirikisho la Kampuni za gesi Afrika Mashariki likiendelea jijini Dar es Salaam

*************************

Na Mwandishi Wetu

WATANZANIA wamehamasishwa kuongeza nguvu katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuondokana na athari mbalimbali zikiwamo za mazingira huku matumizi ya nishati safi ya kupikia yakitajwa kuwa sehemu ya mkakati wa kuendeleza uchumi kuanzia ngazi ya familia na taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Shirikisho la Kampuni za Gesi nchini Tanzania, Araman Benoite ambaye pia ni Mkurugenzi wa Oryx Gas nchini alipokuwa akizungumza kwenye Kongamano la Kampuni za Gesi Afrika Mashariki linaloendelea jijini humo.

"Tutumie fursa ya gesi ya kuwekeza ili kuwafikia wananchi wengi ambao bado hawajaanza kutumia nishati safi ya kupikia. Pia tuitumie fursa hiyo kuwekeza na kuimarisha uchumi," amesema Benoite.

Benoite ameongeza kwamba bado kuna fursa ya uwepo wa soko kubwa la gesi ya majumbani kwani Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipambanua kuhamasisha matumizi yake.

Akizungumzia umuhimu wa kufanyika kwa kongamano hilo amesema ni sehemu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo ina faidi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Benoite, miongoni mwa faida hizo ni pamoja na kusaidia mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira, kuunga mkono jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutumia muda mchache katika shughuli za mapishi tofauti na pale endapo wangetumia nishati nyingine kupikia kama Kuni au mkaa.

Akifafanua kwa nini kongamano hilo limefanyika Tanzania, amesema ni moja ya mkakati wa Kampuni za gesi kuunga mkono jitihada za Serikali inayoongozwa na Rais Samia kufungua fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati ya gesi.

Kongamano hilo limehudhuriwa na wadau kutoka nchi mbalimbali ikiwamo za Jumuiya ya Afrika Mashariki zikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na kampuni za Kimataifa zinazokijusisha na biashara ya gesi duniani.

Awali akisoma hotuba ya ufungui wa kongamano hilo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Mkurugenzi wa Shirikisho hilo duniani Catherine Ho, alisema kongamano hilo litakuwa jukwaa muhimu katika kuongeza uelewa na kukuza uwekezaji katika sekta ya nishati hususan gesi ya majumbani (LPG) nchini Tanzania.

Amesema zaidi ya washiriki 800 walisajiliwa katika kongamano hilo wakiwemo wataalamu wa nishati ambapo pamoja na mambo mengine wataonyesha jinsi sekta hiyo ilivyo muhimu katika kukuza uchumi.

Pamoja na mambo mengine kwenye Kongamano hilo la Kimataifa,pia wameanzisha Shirikisho ngazi ya Tanzania ambalo litakuwa likisimamia na kutoa muongozo kuhusu masuala mbalimbali kwenye sekta ya nishati ya gesi.

Post a Comment

0 Comments