Ticker

6/recent/ticker-posts

WANAWAKE MAHAKAMA WAUNGANA NA WENZAO KUSHEREHEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

-Divisheni ya Ardhi nayo yatoa msaada kwa akina Mama Muhimbili

Na Mary Gwera na Magreth Kinabo

Watumishi wanawake wanaofanya kazi Mahakama ya Tanzania Mkoa wa Dar es Salaam leo tarehe 08 Machi, 2023 wameungana na Wanawake wenzao wa Mkoa huo kusherehekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Viwanja vya Mnazimmoja jijini humo.

Akizungumza na Maelfu ya Wanawake kutoka Ofisi mbalimbali waliokusanyika katika Viwanja vya Mnazimmoja jijini humo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla ametoa rai kwa Watanzania kununua kuwaunga mkono akina Mama wajasiriamali kwa kununua bidhaa zinazozalishwa na wanawake kwani nyingi zinakidhi ubora hata zaidi ya bidhaa zinazotoka nchi za nje.

“Nachukua nafasi hii kuwapongeza wanawake kwa siku hii muhimu kwenu, nami kwa kutambua umuhimu wake nimeona niahirishe shughuli nyingine zote ili nishiriki nanyi, kwa nafasi hii napenda kuwapongeza pia wajasiriamali wanawake kwa bidhaa nzuri na hivyo nawaomba wananchi muwaunge mkono kwa kununua bidhaa hizo,” amesema.

Kadhalika, Mhe. Makalla amewataka Wanawake kuendeleza ushirikiano na mshikamano miongoni mwao ili waweze kupata maendeleo ya dhati na vilevile kuahidi kuwa Serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kutoa ushirikiano husuani mikopo ili kuwawezesha wanawake kuendelea na shughuli za uzalishaji mali.

Mkuu huo wa Mkoa ameongeza kuwa, Mkoa wake utaendelea kuwawezesha kiuchumi wanawake huku akieleza kwamba, Mkoa huo umezindua vikundi mbalimbali vya VIKOBA ambapo kupitia vikundi hivyo wanawake wameweza kukua kiuchumi na kufanya maendeleo kadha wa kadha.

“Naomba mpuuze maneno yanayosemwa na baadhi ya Wanasiasa kuhusu VIKOBA, mtu anayezungumzia vibaya kuhusu VIKOBA hajui umaskini ulivyo na maana, hivyo endeleeni na tutaendelea kuvizindua vingi zaidi,” amesisitiza Mhe. Makalla.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka huu, 2023 inasema; ‘Ubunifu na mabadiliko ya Teknolojia ni chachu katika kuleta usawa wa kijinsia,’.

Wakati huohuo, Watumishi wanawake wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo Mhe. Agnes Mgeyekwa katika kusherekea siku hiyo wameungana wanawake waliolazwa na watoto wao kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kutoa msaada wa vitu mbalimbali.

Wanawake wa Mahakama hiyo wametoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wakinamama hao, ambavyo ni pamoja na sabuni za kuogea na kufulia, mafuta ya kujipaka, miswaki, dawa ya meno, taulo za kike na nepi za Watoto (diapers).

Akizungumzia kuhusu siku hiyo, Jaji wa Mahakama ya Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Arafa Msafiri amesema wanawake wa Mahakama hiyo wametoa msaada wa vitu hivyo, ikiwa ni ishara ya kuonesha upendo kwao.

Vitu hivyo vilikabidhiwa kwa wanawake hao, kupitia Usimamizi wa Parokia ya Muhimbili Somo Bikira Maria Salama ya Wagonjwa) chini ya Padri Athanas Bwakila, ambaye alishukuru kwa msaada huo, huku akisema bado wakinamama wana mahitaji yao ni makubwa na wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo madeni ya matibabu, ambapo aliwaomba watu wengine kuiga mfano huo wa kuwasaidia wahitaji hao.

Padre Bwakila aliwashauri wanawake wote kuwa waadhimishe siku hiyo kwa kukumbushana kulea familia zao vizuri ili ziweze kuwa na maadili mema.

Kwa upande wa Mahakama Kuu Masjala Kuu, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam na Mahakama Kuu Kituo cha cha Usuluhishi wameadhimisha siku hiyo kwa kukumbushana mambo mbalimbali, mgeni rasmi alikuwa ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Dkt.Benhajj Masoud.

Akizungumzia kuhusu siku hiyo, Jaji Masoud alisema ni muhimu kukumbuka na kuzingatia kuwa kila siku ni siku ya wanawake kwa muktadha wa nafasi ya wanawake na mchango wa wanawake katika maendeleo na kila kitu kwenye maisha ya kila mmoja.

‘‘Hata hivyo, tunapoadhimisha siku hii adhimu na muhimu hatuna budi kukumbuka uwepo wa vitendo vya kinyanyasaji na kibaguzi wanavyofanyiwa wanawake kila siku na hivyo uwepo wa haja na kuzidisha kuongeza jitihada na maarifa kwenye vita ya kukabiliana na tatizo hili, zikiwemo changamoto zake,’’amesisitiza huku akisema vita hiyo iwe endelevu.

Jaji Masoud ameongeza kwamba ubunifu na matumizi sahihi ya mabadiliko ya teknolojia yanaifanya teknolojia iondoe vikwazo ambavyo wanawake wengi walikuwa wakikabiliana navyo katika nyanja zote za misha, kijamii, kiuchumi na kisiasa.Pia teknolojia inasaidia kuhabarisha umma kuhusu vitendo vinavyoathiri usawa wa kijinsia na nmna bora ya kukabiliana navyo.

Amesema teknolojia inaleta wepesi wa kufikia na kupata haki na hivyo urahisi wa kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, inaleta wepesi na fursa za kiujasiriamali na ajira.

Wanawake hao pia walikumbushana kuwa na umiliki wa mali, ubunifu, kujiamini, kushirikiana na kujenga uthubutu wa kufanya mambo mbalimbali.

MATUKIO KATIKA PICHA MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI MKOA WA DAR ES SALAAM


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mkoa wa Dar es Salaam akitoa hotuba yake wakati wa Sherehe hizo zilizofanyika leo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Katika picha ni sehemu ya Watumishi Wanawake wanaofanya kazi Mahakama ya Rufani wakiwa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam zilipofanyika Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani leo tarehe 08 Machi, 2023.
Sehemu ya Watumishi wanawake wa Mahakama ya Rufani (T) wakiwa katika picha ya pamoja katika Viwanja vya Mnazi Mmoja zilipofanyikia sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kimkoa.
Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu (ADHR)-Mahakama ya Tanzania, Bi. Agnes Kavishe (katikati) akikata keki maalum iliyoandaliwa kwa Watumishi Wanawake wa Mahakama ya Rufani ikiwa ni ishara ya kusherehekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. Wanaoshuhudia ni Maafisa Utumishi wa Mahakama.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Rufani Wanawake wakiwa kwenye hafla fupi ya kusherehekea Siku ya Wanawake Dunia iliyofanyika katika Ukumbi wa Maktaba uliopo katika Mahakama hiyo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Arafa Msafiri (aliyenyoosha mikono) akizungumza na baadhi ya wakina mama waliolazwa na watoto wao katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili leo wakati Watumishi wanawake wa Divisheni hiyo walipofika hospitalini hapo kwa ajili ya kutoa msaada wa vitu mbalimbali. Katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agness Mgeyekwa na kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Dkt. Theodora Mwenegoha.
Baadhi ya vitu mbalimbali vilivyotolewa msaada na Mahakama hiyo kwa wakina mama waliolazwa na watoto wao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Padri Atanas Bwakila (mwenye joho jeupe) akizungumza na baadhi ya wanawake Mahakama hiyo.
Baadhi ya wanawake wa Mahakama hiyo wakimsikiliza Padri.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agatha Chugulu akitoa neno la Shukrani.
Mkuu wa Wanachuo wa Chuo Kikuu cha Tumaini (TUDARCo), Bi. Lois-Singa Metili akitoa Mada ya Ujasiriamali na Ubunifu kwa Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi wakati ikiwa ni sehemu ya kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani leo tarehe 08 Machi, 2023.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agness Mgeyekwa (katikati) pamoja na sehemu ya Watumishi wa Divisheni hiyo wakikata keki kusherehekea Sikukuu ya Siku ya Wanawake Duniani.
Baadhi ya wanawake wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam na Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi wakifurahia leo Siku ya Wanawake Duniani katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Dar es Salaam.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi Mhe. Dkt. Benhaji Masoud aliyekuwa Mgeni rasmi katika hafla hiyo akizungumza na Wanawake hao. (wa tatu kushoto) ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sekela Moshi,wa kwanza kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Salma Maghimbi, (Wa pili kulia) ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, Mhe. Leila Mgonya na wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Zainabu Mango, wa pili ni kushoto Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Elizabeth Mkwizu.

Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sekela Moshi, akizungumza jambo katika hafla hiyo.
Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sekela Moshi (kulia), akimlisha keki mgeni rasmi Mhe. Dkt. Benhaji Masoud wakati wa hafla fupi ya kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani.


Post a Comment

0 Comments