Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YASAINI MKATABA WA BILIONI 3.8 KUJENGA KIVUKO KIPYA BUYAGU MBALIKA

Na. Alfred Mgweno (TEMESA) Sengerema Mwanza

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), leo Tarehe 23 Aprili, 2023 imesaini Mkataba wa ujenzi wa kivuko kipya kitakachogharimu shilingi Bilioni 3.8 mpaka kukamilika kwa ajili ya kutoa huduma katika maeneo ya Buyagu na Mbalika Wilaya za Sengerema na Misungwi Mkoani Mwanza.

 Hafla ya utiaji saini mkataba huo ambao Serikali imesaini na Kampuni ya Kizalendo ya Songoro Marine Transport Limited ya jijini Mwanza, imefanyika katika viwanja vya Sabasaba Wilayani Sengerema na kushuhudiwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya ambaye alikua mgeni rasmi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhandisi Kasekenya ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi ambavyo imetoa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi hususan miradi ya vivuko na kusema kuwa ujenzi wa Kivuko hicho ni juhudi ya Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha huduma kwa jamii kwa kuwapatia miundombinu yenye uhakika ya usafiri.

‘’Ujenzi wa kivuko hiki utakapokamilika utaharakisha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa wananchi waishio katika Wilaya ya Sengerema, Misungwi na maeneo mengine, aidha inatarajiwa kuwa na usafiri wa uhakika wenye huduma bora na salama katika maeneo ya Buyagu na Mbalika.’’ Amesema Kasekenya na kuwaagiza TEMESA kusimamia mradi huo kwa ukaribu ili kivuko hiki kiweze kujengwa kwa ufanisi mkubwa na kwa wakati.

‘’Gharama ya ujenzi wa kivuko hiki ni kubwa hivyo, ninaomba tuzingatie thamani ya fedha (Value for Money) wakati wa utekelezaji wa Mradi huu.’’ Alisisitiza Naibu Waziri na kuongeza kuwa madhumuni ya ujenzi wa kivuko hicho ni kuwapatia usafiri ulio salama na wenye uhakika wananchi wa maeneo hayo ambao wamekuwa wakitumia mitumbwi kwenye eneo hilo lenye takribani kilometa saba (Nautical Miles 3.7).

Awali, akisoma taarifa fupi ya mradi, Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Lazaro N. Kilahala amesema hitaji la kivuko cha uhakika baina ya Buyagu na Mbalika limekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa maeneo hayo hivyo Ujenzi wa kivuko hicho utakapokamilika utaondoa kero nyingi za kiuchumi na kijamii ambazo zimekuwa zikichelewesha maendeleo ya wananchi hao hivyo kutimiza azma ya Serikali kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Kilahala amesema Ujenzi wa vivuko vipya na ukarabati wa vivuko pamoja na miundombinu yake ni muendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025.

‘’katika mwaka huu wa fedha, Wakala unaendelea na Ujenzi wa vivuko vipya vitano vyenye thamani jumla ya shilingi Bilioni 33.2 vitakavyotoa huduma kwenye vituo vya Kisorya - Rugezi, Bwiro – Bukondo, Nyakarilo – Kome, Ijinga – Kahangala na Mafia – Nyamisati hivyo kivuko cha Buyagu-Mbalika ambacho leo mkataba wake wa Ujenzi umesainiwa ni kivuko cha sita (6) ambacho Ujenzi wake unaanza katika mwaka huu wa fedha.‘’Amesema Kilahala na kuongeza kuwa sambamba na Ujenzi wa vivuko vipya katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali kupitia Wakala inafanya ukarabati wa vivuko 18 pamoja na Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vivuko katika maeneo 11 ya huduma kwa gharama ya shilingi bilioni 27.5.

Naye Mbunge wa Misungwi Mhe. Alexander Mnyeti akizungumza kwenye tukio hilo ametoa pongezi kwa Mhe. Rais wa Tanzania kwa kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi ambayo inaenda kunufaisha wakazi wa maeneo mbalimbali nchini.

‘’Kwa kwa niaba ya wananchi wa Misungwi nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi anazoendelea kuzifanya kwenye majimbo yetu ya Kanda ya Ziwa, sisi wakazi wa Misungwi ni mashahidi kwamba tumepokea fedha nyingi za miradi mingi sana.’’Amesema Mnyeti.

Mbunge wa Sengerema Mhe. Hamis Tabasam naye akizungumza kwenye hadhara hiyo naye amewataka wananchi wa Wilaya ya Sengerema kuishukuru Serikali kwa miradi hiyo ambayo inatekelezwa katika Wilaya yao, ‘’ahadi za viongozi Serikali imetekeleza, nawashukuru sana, wana Sengerema tumshukuru sana Mhe. Rais, namshkuru sana Mhe. Mbarawa, namshkuru sana Katibu Mkuu Ujenzi, miradi inatekelezwa hakuna kinachosimama.’’ Amesema Mhe. Tabasam.

Mtendaji Mkuu TEMESA Lazaro Kilahala, ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kukubali kuanza utekelezaji wa mradi huo na mingine na kuahidi kufanya kazi kwa weledi na jitihada kubwa ili kufikia malengo na matarajio ya Serikali na wanachi kwa ujumla.

Kivuko cha Buyagu Mbalika kitakapokamilika kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kubeba tani 50 zikijumuisha; abiria 100 (waliokaa 50 na waliosimama 50) pamoja na magari madogo (saloon cars) 6.





Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro Kilahala kushoto akisaini mkataba wa ujenzi wa Kivuko kipya cha Buyagu Mbalika na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Major Songoro kulia katika hafla fupi ya utiaji saini iliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza leo. Wanaoshuhudia nyuma yao ni Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Godfrey Kasekenya na nyuma ya Kilahala ni Mbunge wa Misungwi Mhe. Alexander Mnyeti na kulia ni Mbunge wa Sengerema Mhe. Hamisi Tabasam na Mbunge wa Buchosa Mhe. Erick Shigongo. Kivuko cha Buyagu Mbalika kitakapokamilika kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kubeba tani 50 zikijumuisha; abiria 100 (waliokaa 50 na waliosimama 50) pamoja na magari madogo (saloon cars) 6.







Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro Kilahala kushoto na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Major Songoro wakionyesha mikataba waliyosaini ya ujenzi wa kivuko kipya cha Buyagu Mbalika katika hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza leo. Wanaoshuhudia nyuma yao ni Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Godfrey Kasekenya na nyuma ya Kilahala ni Mbunge wa Misungwi Mhe. Alexander Mnyeti na kulia ni Mbunge wa Buchosa Mhe. Erick Shigongo. Kivuko cha Buyagu Mbalika kitakapokamilika kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kubeba tani 50 zikijumuisha; abiria 100 (waliokaa 50 na waliosimama 50) pamoja na magari madogo (saloon cars) 6.


Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Godfrey Kasekenya akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Sengerema leo wakati wa hafla fupi ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Kivuko kipya cha Buyagu Mbalika iliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza. Kivuko cha Buyagu Mbalika kitakapokamilika kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kubeba tani 50 zikijumuisha; abiria 100 (waliokaa 50 na waliosimama 50) pamoja na magari madogo (saloon cars) 6.

Post a Comment

0 Comments