Ticker

6/recent/ticker-posts

TAASISI ZATAKIWA KUACHA MATUMIZI YA KUNI NA MKAA ILI KUPUNGUZA UKATAJI WA MITI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na waandishi wa habari lhawapo pichani) leo Aprili 12, 2023 jijini Dodoma kuhusu katazo la matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kwa taasisi za umma na binafsi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 12, 2023 Jijini Dodoma kuhusu katazo la matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kwa taasisi za umma na binafsi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo akizungumza na waandishi na waandishi wa habari leo Aprili 12, 2023 Jijini Dodoma kuhusu katazo la matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kwa taasisi za umma na binafsi. Katikati ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Bw. Abdallah Hassan Mitawi na Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Dkt. Thomas Bwana.

(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)

**********************

Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imezitaka Taasisi zote za Umma na Binafsi Tanzania Bara zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 100 kwa siku kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 31, 2024.

Pia, imezielekeza taasisi zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 300 kwa siku kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 31, 2025.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo April 12, 2023 jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo amesema Serikali inazihimiza taasisi hizo kwa sasa kutumia nishati mbadala ambayo ni safi kwa ajili ya kupikia.

“Kwa Mamlaka niliyopewa chini ya Kifungu cha 13 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191, natoa Katazo Kwa Taasisi zote za Umma na Binafsi Tanzania Bara zinazoandaa chakula na kulisha watu kuacha matumizi ya mkaa na kuni,” amesisitiza Dkt. Jafo.

Waziri Jafo amesema watumiaji wakubwa wa nishati za kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia ni taasisi za umma na binafsi, hivyo kutokana na athari zake kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi, Serikali imeandaa Dira ya Taifa ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia pamoja na Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Dira hiyo kwa kipindi cha miaka kumi hadi kufikia 2033.

“Pamoja na urahisi na unafuu wa upatikanaji wa nishati hiyo, matumizi ya kuni na mkaa yanaathiri afya ya mtumiaji kwa kusababisha magonjwa yatokanayo na kuvuta hewa chafu ambayo huathiri mapafu, moyo na matumizi ya muda mrefu wa nishati hiyo pia husababisha magonjwa ya macho,” amesema Dkt. Jafo.

Ameongeza kuwa Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira nchini ya mwaka 2019 inaonesha kuwa kasi ya uharibifu wa misitu ni kubwa na kila mwaka zaidi ya hekta 469,420 huharibiwa kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.

Waziri Jafo amefafanua kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizopo inakadiriwa kuwa asilimia 16 ya ardhi imeharibika na inakabiliwa na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame kutokana na watu wengi kufanya shughuli zisizo endelevu ikiwemo kutumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia kutokana na nishati hiyo kupatikana kwa urahisi na watu wengi wanaweza kumudu gharama yake.

Akifafanua zaidi Dkt. Jafo amesema kutokana na athari hizo zilizojitokeza, kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kujenga uchumi wa viwanda, hivyo matumizi ya nishati mbadala ikiwemo mkaa mbadala yatatoa fursa ya viwanda vya kutengeneza mkaa mbadala sanjari na kuzalisha majiko sanifu na banifu kwa ajili ya matumizi fanisi ya nishati hiyo.

Hivyo, ametoa wito kwa makampuni ya gesi, mkaa mbadala na majiko banifu yatumie katazo hili kama fursa ya uzalishaji wa bidhaa hizo kwa wingi kwa ajili ya kupanua wigo wa masoko kwa taasisi hizo.

Itakumbukwa kuwa Juni Mosi 2021, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alitoa tamko la Wiki ya Mazingira Duniani na kuzielekeza Taasisi, Mashirika ya Serikali na Sekta Binafsi zianze kutumia nishati mbadala kwa kupikia na shughuli nyingine za uzalishaji.


Post a Comment

0 Comments