Ticker

6/recent/ticker-posts

CHALAMILA AIBUKIA MWENGE DAR AZUNGUMZA NA WAFANYABIASHARA


MKUU wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amefanya ziara ya Kushtukiza katika Soko la Mwenge ikiwa ni mara yake ya kwanza kufanya hivyo baada ya kuhamishwa kituo cha kazi na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutoka mkoani Kagera.

Akizungumza mara baada ya kufika katika Soko hilo Leo Mei 16, 2023 RC Chalamila amesema, dhamira ya kupita kwenye maduka mbalimbali ni Kujionea hali halisi ya kinachozungumzwa na wafanyabiashara mitaani.

"Pamoja na kuwa Sijaingia Ofisini rasmi lakini nimeona ipo haja ya Kusikia hasa huku mtaani watu wanasema nini, lakini katika moja eneo nililopita watu wanalalamikia uwepo wa kodi kubwa zisizoweza kulipwa na Wafanyabiashara kutokana na Kiwango kikubwa cha VAT ambayo ni asilimia 18" amesema Chalamila.

Aidha RC Chalamila amesema Suala lingine ambalo linalalamikiwa na Wafanyabiashara hao ni kuhusiana na Idara ya Forodha ambayo imeweka viwango vikubwa vya Kodi hasa katika Vitenge pamoja na mlolongo mrefu wa Ufuatiliaji ambapo ni kikwazo kwa wafanyabiashara wengi.

"Jambo la tatu ambalo nimelisikia ni kuwepo kwa zoezi la kamata kamata kwa Wafanyabiashara Kariakoo na kuwakosesha Uhuru pamoja na kuleta usumbufu kwa wateja wao na hasa kwa wateja kutoka Kongo, Zambia, Malawi pamoja na mataifa mengine" ameeleza RC Chalamila.

Pia Mkuu huyo wa mkoa amesema alichobaini kwa Wafanyabiashara katika eneo la Mwenge ni Kuwepo kwa wafanyakazi wanafunzi ambao wanatumiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao wanakuwa hawana uwezo wa lugha nzuri na yenye staha kwa Wafanyabiashara.

"Jambo lingine ni Utaratibu wa TRA kuruhusu mizigo kutoka Bandarini na Baadae tena Wanakuja Kukagua nyaraka Sehemu za Kuhifadhia mizigo (Godown), jambo ambalo wafanyabiashara wanasema ni usumbufu mkubwa kwao"

Pamoja na hayo amesema amekutana na malalamiko ya uwepo wa kukithiri kwa rushwa kwa baadhi ya watendaji wa TRA na kwa wafanyabiashara wanaopanga bidhaa zao chini wanalalamika kukosekana kwa maeneo.

"Kubwa zaidi ni Kauli ya Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya Kusamehe Kodi ya Miaka mitatu au Mitano nyuma, ambapo Wafanyabiashara hawajaweza kuichukua kauli ya Rais Kwa Vitendo, ambao Sasa TRA wamekuwa wakiomba Barua Rasmi kutoka kwenye Mamlaka hizo kwa Maana ya Rais, Waziri Mkuu au Makamu wa Rais" amebainisha RC Chalamila.

Amesisitiza kuwa azma ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan itatimia na itakwenda vizuri na kila jambo ambalo linaendelea kwa wafanyabiashara wa Kariakoo litaisha kwa usalama.

Post a Comment

0 Comments