Ticker

6/recent/ticker-posts

EXPEDIA GROUP KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KUTANGAZA UTALII

Seattle, Marekani

Kampuni kubwa ya biashara ya utalii duniani kupitia mtandao, Expedia Group, imeahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Bodi ya Utalii (TTB), kutangaza na kuleta watalii wengi zaidi nchini Tanzania.

Kauli hiyo inayounga mkono pia juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuitangaza Tanzania kimataifa, imetolewa jana Mei 8, 2023, na Mkurugenzi Mwandamizi wa Masoko ya Kimataifa wa kampuni hiyo, Bw. Andrew Van Der Feltz, alipokutana na kufanya mazungumzo kwenye makao makuu yao mjini Seattle na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi.

Expedia ni kampuni inayotumia teknolojia za kisasa kutangaza na kuhudumia watu zaidi ya milioni 400 kwa mwezi duniani na ikiwa inatumia muunganiko wa zaidi ya tovuti 200 na ikifanya kazi na mashirika ya ndege na wabia wengine zaidi ya 509 ikishika nafasi ya pili duniani na wakati fulani namba moja Marekani kwa kuaminiwa na watalii katika sekta ya usafiri na utalii.

Awali, ujumbe wa Tanzania pia ulipata wasaa wa kusalimiana na Rais wa Expedia Group anayeshughulikia Biashara ya Kimataifa, Bi. Ariane Gorin, ambaye aliueleza ujumbe huo kuwa Tanzania ambako alipata kutembelea mwaka 2016 Tarangire, Serengeti na Ngorongoro Kreta kuwa ni nchi yenye vivutio vya kipekee na anatarajia kuitembelea tena.

Kwa upande wake Dkt. Abbasi aliyeambatana na Mtendaji Mkuu wa TTB, Damasi Mfugale, aliwahakikishia watendaji hao wa Expedia kuwa Tanzania kwa sasa imeamua kuja na mtazamo mpya katika kutangaza utalii.

“Tunaamini utaalamu wenu na uzoefu wenu katika masoko na biashara ya utalii kimtandao utasaidia kuongezea juhudi za Rais wetu wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amefanya juhudi kubwa kupitia filamu ya “Tanzania; The Royal Tour” kuiweka Tanzania katika taswira pana zaidi kimataifa katika utalii na uwekezaji,” alisema Dkt. Abbasi.






Post a Comment

0 Comments