Ticker

6/recent/ticker-posts

KAMILISHENI MIRADI KWA WELEDI

Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu amewaasa viongozi wa Wilaya ya Chamwino kukamilisha miradi kwa wakati pamoja na kuzingatia ubora unaokidhi viwango vinavyotakiwa.

Maagizo hayo yametolewa leo tarehe 18/05/2022 na Bw. Gugu alipofanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali katika Halmashauri ya Chamwino na kuongea na watumishi wa wilaya hiyo kwa lengo la kuweka mikakati bora ya utendaji kazi ili kutimiza azma ya maendeleo kwa uharaka.

"Tuna miradi ambayo inatakiwa kukamilika kwa muda mfupi ikiwemo miradi ya fedha za boost ambayo inatakiwa kukamilika hadi kufikia Juni 30, 2023 kwa hiyo viongozi tuhamasishane kutekeleza miradi hii kwa wakati na ubora unaotakiwa kwa muda mfupi lakini kwa weredi wa hali ya juu pamoja na kuzingatia kanuni zote za Serikali ili kuepukana na hati chafu zinazotokana na upotevu wa nyaraka mbalimbali za manunuzi" Gugu amesisitiza.

Hata hivyo Bw. Gugu amewausia watumishi wa Wilaya hiyo kuwa waadilifu kazini, kudumisha ushirikiano, kuheshimiana bila kujali nyadhifa walizonazo pamoja na kupendana ili kurahisisha utendaji kazi ikiwa ni pamoja na kutatua matatizo ya wananchi ngazi ya Wilaya kwa yale ambayo hayahitaji ngazi ya Mkoa kupata suluhu zake.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi – Utawala na Utumishi Mkoa wa Dodoma Bi. Coletha Kiwale amepongeza juhudi za mwelekeo wa kumalizika kwa miradi mbalimbali ikiwemo Zahanati ya Kijiji Cha Wilunze ambayo imefikia hatua ya umaziaji.

Katika ziara hiyo ya kikazi katibu Tawala amekagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ofisi za Wilaya ya Chamwino, Zahanati ya Kijiji Cha Wilunze na Mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya maabara ya kemia na baiolojia katika Shule ya Sekondari Msanga ambavyo ujenzi wake unaendelea.
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu akikagua jengo la vyumba viwili vya maabara ya kemia na baiolojia vya Shule ya Sekondari Msanga katika ziara yake ya kikazi Wilaya ya Chamwino tarehe 18/05/2023. Katika ukaguzi huo Bw. Gugu ametoa rai kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chimwino kukamilisha ujenzi wa madarasa hayo kwa wakati.
Watumishi wa Wilaya ya chamwino wakimsikiliza na kutoa maoni yao mbele ya na katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu (hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chamwino jana.
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu akikagua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Chamwino alipofanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuongea na watumishi wa Ofisi ya Wilaya hiyo hivi karibuni.
Jengo la Zahanati ya kijiji cha Wilunze linalojengwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Wilaya ya Chamwino linalogharimu takribani milioni 92 hadi kukamilika kwake.


Post a Comment

0 Comments