Ticker

6/recent/ticker-posts

KATAMBI: THAMANI YA UWEKEZAJI WA MIFUKO YA HIFADHI JAMII IMEFIKIA TRIL.14/-

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi (Mb) akijibu swali Bungeni leo tarehe 16 Mei, 2023, jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu, DODOMA Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Patrobas Katambi amesema hadi kufikia Juni 30, 2022 thamani ya uwekezaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ilikuwa imefikia Sh.Trilioni 14.04.

Mhe.Katambi ameyasema hayo Mei 16, 2023 bungeni alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti maalum (Chadema), Halima Mdee.

Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji tangu kuanzishwa kwa Mifuko hiyo ni kiasi gani cha fedha kimewekezwa na kila Mfuko na nini faida na hasara za uwekezaji huo.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Katambi amesema kiwango hicho ni kwa mujibu wa hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambapo katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ulikuwa umewekeza Sh.Trilioni 6.03, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Sh.Trilioni 7.49 na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Sh.Bilioni 521.94.

Ametaja faida za uwekezaji huo kuwa ni kulinda thamani ya michango ya wanachama na kuhakikisha Mifuko inakuwa endelevu ili kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulipa mafao.

“Aidha, uwekezaji huu huchangia pia kuongeza ajira, mapato ya Serikali kupitia kodi na kuchochea shughuli za uchumi,”amesema.


Hata hivyo, amesema kama ilivyo katika uwekezaji wowote kuna vihatarishi amabavyo vinaweza kusababisha hasara kwa baadhi ya uwekezaji, ambapo mifuko imevifanyia kazi kwa mujibu wa miongozo ya uwekezaji katika mifuko inayotolewa na Benki kuu ya Tanzania (BOT).


Post a Comment

0 Comments