Ticker

6/recent/ticker-posts

SPIKA DKT.TULIA AIPA NENO TTCL


SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dk Tulia Ackson,akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua mabanda mbalimbali katika Maonesho yanayoendelea viwanja vya Bunge Jijini Dodoma leo Mei 18,2023.

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dk Tulia Ackson,akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),Mhandisi Peter Ulanga wakati alipotembelea banda la Shirika hilo katika Maonesho yanayoendelea viwanja vya Bunge Jijini Dodoma leo Mei 18,2023.Kushoto ni Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Mathew Kundo.


Meneja Biashara TTCL Dodoma Bi.Leyla Pongwe,akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la shirika hilo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),Mhandisi Peter Ulanga wakati katika Maonesho yanayoendelea viwanja vya Bunge Jijini Dodoma leo Mei 18,2023. 

 SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dk Tulia Ackson,amelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuvitangaza vivutio vya utalii vya Tanzania . 

Spika Dkt.Tulia ameyasema hayo leo Mei 18,2023 katika banda la shirika hilo wakati maonesho ya baadhi ya Huduma na bidhaa wanazotoa yanayofanyika katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma. 

Dkt.Tulia amesema kuwa uwepo wa huduma za mawasiliano zinaimarisha shughuli za ulinzi na usalama kwa watalii wakiwa mlimani kupitia mamlaka husika jambo ambalo ni kivutio cha kuchochea uchumi wa kidigiti. 

“Tumeona mmefika Kilimanjaro,hiyo itakuwa nzuri kwa sababu kutakuwa hakuna uongo uongo,piga tujue umefika kileleni kama mmefika pale ni vizuri nawaongeza sana mnafanya kazi nzuri,”amesema Spika Tulia.

 Hata hivyo ameipongeza pia kuunganisha mkongo kufika nyumbani ni jambo la muhimu kwani matumizi ya data na teknolojia ni muhimu.

“Nitume nafasi hii kuwapongeza TTCL kwa kutuleta huduma hii naamini zitapunguza gharama ya matumizi ya bando ambayo tumekuwa tunalalamika.

Aidha ameipongeza Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kuleta maonesho hayo katika viwanja vya Bunge ili wabunge waone wenyewe yanayoendelea katika maeneo yao ya uwakilishi.

Kwa upande wake Meneja Biashara TTCL Dodoma Bi.Leyla Pongwe,ameeleza lengo la kushiriki katika maonesho hayo kuwa ni kuwaonesha wabunge mikakati ambayo wamejiwekea katika kusaidia serikali kufikia uchumi wa kidigitali mpaka kufikia mwaka 2025.

 “Katika shughuli ambazo tumeleta kuonesha hapa kwanza tumeweza kurahisisha utalii baada ya kuweza kufikisha mawasiliano katika miaka 61 ya uhuru tumewezesha kufikisha mawasiliano katika kilele cha mlima kilimanjaro(Uhurupeak) na hiki ndiyo kilele cha Afrika mashariki kwasababu ukisimama pale juu unauwezo wa kuona Afrika mashariki yote.

“Zamani ilikuwa mtalii akipanda juu anakuwa hapatikanai ila sasa hivi mtalii anapatikana.Sasa hivi tunamletea mtanzania fiber mpaka nyumbani kwake analipia kifurushi kwa mwezi kwani ili kufikia uchumi wa kati lazima uwe na intaneti,”amesema

Maonesho ya wadau wa Mawasiliano yanaendelea kwa siku 3 katika viwanja vya bunge ikiwa ni kuelekea kwenye bunge la bajeti ya Mawasiliano linalotarajiwa kusomwa kesho na Waziri wa Habari na Mawasiliano Mheshimiwa Nape Mnauye.

Post a Comment

0 Comments