Ticker

6/recent/ticker-posts

WADAU WASHAURI SERA MPYA YA ELIMU KUANZISHWA SHULE MAALUMU ZA UFUNDI ZA KULEA VIPAJI



Na.Alex Sonna-DODOMA

KATIKA Mijadala ya kutoa maoni ya maboresho ya Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 wadau wameshauri kuwepo kwa shule maalumu za ufundi za kulea vipaji mbalimbali ili kuondoa dhana ya wahitimu kutegemea kuajiriwa pekee.

Wadau hao wametoa maoni hayo wakati wa kongamano la kujadili sera na mitaala mipya ya elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu linaloendelea jijini Dodoma.

“Mfano shule inayojikita katika michezo sio lazima tusubiri mtoto awe ngazi ya sekondari anakuwa na miaka labda 15 lakini ukitaka upate mwanamichezo bora ni lazima mtoto aandaliwe tangu akiwa mdogo maana yake ziandaliwe shule maalumu na sio mchanganyiko itakayokuwa na walimu wa michezo na watoto wafundishwe tangu akiwa mdogo” amesema Siston Masanja.

Amebainisha kuwa maandalizi ya shule maalumu yaendane pia na kuwaandaa walimu watakaokuwa wamebobea katika taaluma ya ujunzi au vipaji vinavyofundishwa katika shule hizo.

Wengine wameshauri maboresho hayo yaendane na kuanza kuzalisha walimu watakaokuwa na uelewa juu ya mabadiliko yatakayopitishwa ili kuepuka mkanganyiko mara baada ya kuanza kutumika na walimu wanakuwa hawana uelewa juu ya mabadiliko hayo.

Kwa upande Wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt. Francis Michael ameshauri mabadiliko ya mitaala yazingatie kuwapunguzia mzigo wa masomo kwa wanafunzi kwani kwa sasa kuwa kuwa na masomo mengi ambayo yanaweza kuwa mzigo mkubwa kwa wanafunzi.

“Niliwahi kutembelea nchi moja kuna mhandisi ndie anayetegemewa na nchi hiyo lakini ukimuuliza kuhusu mgawanyo wa majimbo katika nchi yake hana uelewa hii inamaana mtoto anatiliwa mkazo kwenye baadhi ya masomo atakayoyachagua” amesema Dkt. Francis.

Aidha wadau wengine wameshauri mabadiliko ya sera na mitaala ya elimu izingatie elimu ya watu wenye mahitaji maalumu kuanzia kwenye miondombinu na vifaa vya kujifunzia ili watoto wenye mahitaji maalumu waweze kutimiza malengo yao.

Katika hatua nyingine wametaka mabadiliko ya mitaala ya elimu ilenge kuandaa mitihani maalumu hasa kwa watoto wenye mahitaji maalumu katika ngazi za ufundi kwani kuna baadhi ya wanafunzi wanafanya vizuri katika vitendo lakini kwenye nadharia hawafanyi vizuri kutokana na ulemavu walionao.

Post a Comment

0 Comments