Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU ALITAKA BARAZA LA MICHEZO LA UMOJA WA AFRIKA KUKUZA MICHEZO

*Rais Dkt. Samia aipigia chapuo Tanzania kuchaguliwa kuwa Makao Makuu ya Sekretariat ya Baraza hilo.

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka Mawaziri wa michezo wa Baraza la Michezo la Umoja wa Afrika Kanda ya Nne kuweka nguvu katika kuhakikisha wanakuza na kuendeleza michezo kwa Ukanda huo.

Amesema hayo leo Alhamisi (Mei 04, 2023) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa Michezo wa Baraza la Michezo la Umoja wa Afrika Kanda ya IV Jijini Arusha.

Amesema kuwa mawaziri hao wawekeze kwenye kujenga uwezo wa kitalaamu ili kuzalisha wanamichezo wanaoweza kuleta mageuzi kwenye Sekta ya Maendeleo ya Michezo na Maendeleo kupitia Michezo “Tusikubali kushika mkia kila siku na wala tusikubali kurudi nyuma”.

Amesema kuwa lengo la kila taifa ni kuona timu yake inashinda makombe ya Kimataifa hasa Kombe la Dunia. “Tukiamua kuwekeza kwenye miundombinu ya michezo na ujuzi pamoja na kushirikiana tunaweza kufikia malengo makubwa kwenye sekta ya michezo”

“Tunapaswa kufika mahali pa kuona kuwa Tanzania ikishinda wote tumeshinda, Uganda ikishinda, wote tumeshinda, Ethiopia ikishinda wote tumeshinda. Tushirikiane ili tuwe mfano na kielekezo kwa Kanda nyingine za Mabaraza ya Michezo ya Umoja wa Afrika”.

Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wajumbe wa mkutano huo kuichagua Tanzania kuwa makao makuu ya Sekretarieti ya Baraza la Michezo la Umoja wa Afrika Ukanda wa IV katika uchaguzi utakaofanyia mapema leo Mei 04, 2023.

Amewaeleza wajumbe hao kuwa Tanzania ina kila sababu ya kupigiwa kura ya ndiyo kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuipa hadhi sekta ya michezo nchini.

Amesema kuwa uwepo wa mageuzi makubwa katika diplomasia ya michezo ya kimataifa ambapo chini ya uongozi thabiti wa Serikali timu za Taifa za Tanzania na vilabu zinafanya vizuri katika mashindano ya Kimataifa “jambo hili linatia hamasa kwa wanachama kuona kuwa Tanzania inapiga hatua katika kuendeleza sekta ya michezo nchini”

“Uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali kwenye Miundombinu ya Michezo ikiwemo ujenzi wa Viwanja Vikubwa na vizuri vya Michezo vinavyokidhi viwango vya Kimataifa vya CAF na FIFA. Mathalan, Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa ambao hutumiwa kwa Michezo ya Kitaifa na Kimataifa ikiwemo Timu ya Taifa ya Brazili na Klabu ya Everton ambazo pia zimewahi kuutumia”

Katika Mkutano huo, Rais Dkt. Samia Aliwasilisha ujumbe maalumu kwa wajumbe na Mawaziri wa michezo wa Baraza la Michezo la Umoja wa Afrika Kanda ya Nne kuichagua Tanzania kuwa makao makuu ya Sekretarieti ya Baraza la Michezo la Umoja wa Afrika Ukanda wa IV.

“Niwahakikishie kuwa Tanzania inauzoefu wa kuwa makao makuu ya taasisi mbalimbali za kimataifa, na pia Tanzania ina miundombinu yote muhimu ambayo itaiwezesha baraza hilo kufanya kazi kwa ufanisi” Amesema Rais Samia.

Naye Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Balozi Dkt Pindi Chana amesema kuwa tasnia ya michezo ni kati ya sekta ambazo inatoa ajira kwa vijana wengi “sekta ya michezo kwenye nchi wanachama ilitunga sheria ili kuendelea vipaji, michezo inaiunganisha Afrika kuwa moja”

Ameongeza kuwa wataendeleza mapitio ya sheria kanuni na taratibu ili kuendelea kuikuza sekta ya ya michezo kwa kuwa michezo ni biashara na chanzo cha uhakika cha ajira kwa vijana.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na washiriki wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Michezo katika Kanda ya IV ya Afrika (AU Sports Council of Ministers Meeting – Region IV) wakimsikiliza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassanwakati alipowahutubia kwa njia ya video, Mei 4,2023.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Michezo katika Kanda ya IV ya Afrika (AU Sports Council of Ministers Meeting – Region IV) kwenye ukumbi wa Hotel ya Gran Melia jijini Arusha, Mei 4, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dkt. Pindi Chana (wa pili kulia), Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma (kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Said Yakub (wa pili kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela kabla ya kufungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Michezo katika Kanda ya IV ya Afrika (AU Sports Council of Ministers Meeting – Region IV), Mei 4, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahia ngoma ya asili ya Wamasai wakati alipowasili kwenye viwanja vya ukumbi wa Hotel ya Gran Melia jijini Arusha kufungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Michezo katika Kanda ya IV ya Afrika (AU Sports Council of Ministers Meeting – Region IV), Mei 4, 2023. Kushoto ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dkt. Pindi Chana. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro akiwa njiani kwenda Arusha kufungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Michezo katika Kanda ya IV ya Afrika (AU Sports Council of Ministers Meeting – Region IV) kwenye ukumbi wa Hotel ya Gran Melia jijini Arusha, Mei 4, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Post a Comment

0 Comments