Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewapongeza mwanasoka wa kulipwa wa kimataifa Mbwana Samatta na Mwanamuziki nyota Ali Kiba kwa kuanzisha na kuendesha taasisi isiyo ya kiserikali ya SAMAKIBA Foundation ambayo kila mwaka imekuwa ikisaidia masuala mbalimbali katika jamii.
Dkt Kikwete ametoa pongezi hizo katika hafla ya kukabidhi vifaa vya uzazi Pamoja na mashine maalumu za kusaidia Watoto waliozaliwa kabla ya muda wao iliyofanyika katika uwanja wa michezo wa Azam Complex katika kitongoji cha Chamazi wilaya ya Temeke mkoani Dar es salaam Jumanne Juni 20, 2023.
Hafla hiyo, ambayo ni ya sita toka kuundwa kwa SAMAKIBA Foundation, ilifuatia mchezo wa kirafiki wa hisani wa soka kati ya Team Samatta na Team Kiba zinazoundwa na marafiki wa nyota hao wawili, wengi wao wakiwa wachezaji wakubwa wa vilabu mbalimbali na timu ya Taifa.
Vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni 190 vitapelekwa Kibiti Mkoa wa Pwani na Kigoma.
Kiasi hicho cha pesa kilitokana na mapato ya mchezo huo uliovutia wengi, pamoja na misaada ya wafadhili mbalimbali wakiwemo Benki ya ABSA waliokuwa wafadhili wakuu pamoja na kampuni ya ASAS na Shirika la Ushirikiano na Uratibu la Uturuki liitwalo TIKA.
Dkt. Kikwete pia aliimwagia sifa taasisi ya Doris Mollel Foundation, walioandaa na kuratibu shughuli nzima, akiitaja kama ni taasisi inayojitahidi sana kugusa maisha ya wahitaji mbalimbali.
Rais Mstaafu pia aliwashukuru wafadhili wote Pamoja na klabu ya Azam kwa kujitolea uwanja ambao mamia ya wananchi waliojitokeza walishuhudia Team Samatta ikiifunga Team Kiba mabao 4-2.
Uwanja ulilipuka baada ya Team Kiba kupata bao la pili lililofungwa katika kipindi cha pili, kwani lilikuwa bao lililosherehekewa zaidi ya yote katika mchezo huo. Na mfungaji hakuwa mwingine ila mwanamuziki maarufu Marioo, ama ‘Super Sub,' baada ya ‘hitmaker’ huyo kuonesha uwezo wake mkubwa uwanjani, kama alivyo jukwaani...
Hata hivyo, Rais Mstaafu alitoa changamoto kwa Ali Kiba na Mbwana Samatta Pamoja na Doris Mollel Foundation kwa kuwataka wapeleke misaada kwa jamii katika mikoa mbalimbali na isiishie Kibiti mkoa wa Pwani anakotokea Samatta ama Kigoma nyumbani kwao kina Kiba.
“Mwakani mtapoandaa shughuli kama hii natumai mtapeleka misaada kwenye mikoa mingine”, alisema Dkt. Kikwete.



Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akipokea zawadi toka kwa Bi. Doris Mollel, mwandaaji wa hafla hiyo ya mchezo wa hisani kati ya Team Samatta na Team Kiba uliofanyika Azam Complex Chamazi Jumanne Juni 20, 2023
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiondoka akiwa ameondozana na Bi Filiz Sahinci, Mratibu wa mpango wa Taaisi ya Ushirikiano na Uratibu ya Uturuki iitwayo TIKA baada ya kukabidhi vifaa vya hospitali na kushuhudia mchezo wa hisani kati ya Team Samatta na Team Kiba uliofanyika Azam Complex Chamazi Jumanne Juni 20, 2023

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na Bi Filiz Sahinci, Mratibu wa mpango wa Taaisi ya Ushirikiano na Uratibu ya Uturuki iitwayo TIKA baada ya kukabidhi vifaa vya hospitali na kushuhudia mchezo wa hisani kati ya Team Samatta na Team Kiba uliofanyika Azam Complex Chamazi Jumanne Juni 20, 2023. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Mwanahamisi Munkunda


Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiangalia mchezo wao wa hisani kati ya Team Samatta na Team Kiba uliofanyika Azam Complex Chamazi Jumanne Juni 20, 2023. Pamoja naye toka kulia ni Mkurugenzi wa Michezo Bi. Neema Msitha, Mratibu wa ashughuli hiyo Bi. Doris Mollel, Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Mwanahamkisi Munkunda na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya ABSA Tanzania Bw. Obedi Laiser.



Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa hisani kati ya Team Samatta na Team Kiba uliofanyika Azam Complex Chamazi Jumanne Juni 20, 2023. Pamoja naye ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Mwanahamisi Munkunda (shati jekundu) Mkurugenzi wa Michezo katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Neema Msitha (kushoto) na Mwandaaji wa shughuli hiyo Bi. Doris Mollel, kulia.
PICHA NA JMKF
0 Comments