**********************
Na Shemsa Mussa,Kagera .
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imetangaza rasmi kuisha ugonjwa wa Marburg ambao ulisababisha vifo vya watu sita kutoka katika kata za Matuku na Kanyangereko Mkoani Kagera.
Hii ilikuja baada ya wataalam wa afya hapa nchini kwa kushirikiana na shirika la afya ulimwenguni (WHO) kuthibitisha kuwa mlipuko huo haupo tena katika maeneo hayo.
Akizungumza katika Tukio la kutangaza rasmi kumalizika kwa mlipuko wa Ugonjwa wa Marburg lililofanyika katika ofisi za Mkoa wa Kagera, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alitoa shukrani za pekee kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Viongozi wengine wa Afya hapa nchini, Serikali za Umoja wa Ulaya, Serikali ya Marekani na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na kutangaza kuwa ugonjwa huo umeisha rasmi katika Mkoa Kagera.
"Tanzania ipo salama kwa umoja wetu nguvu zetu na ushirikiano wa pamoja tumeweza kuuthibiti ugonjwa huo na hakuna tena " alisema Waziri Ummy.
Aidha Waziri Ummy kupitia Serikali alitoa Shilingi Milioni tano kwa ajili ya familia ya Mtaalam wa Maabara katika Kituo cha Afya Maruku aliyefariki dunia kutokana na ugonjwa huo huku akieleza kuwa Serikali tayari imeweka mkakati wa kutumia shilingi Bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa vituo maalum vya afya katika maeneo ya mipakani kwa ajili ya uimarishaji na ufuatiliaji wa magonjwa ya milipuko.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Tumaini Nagu, akitoa taarifa fupi juu ya mwenendo wa Ugonjwa huo alisema mnamo Machi 16 mwaka huu, ugonjwa huo uliibuka katika Kata za Maruku na Kanyangereko zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera na mgonjwa wa mwisho alipona aprili 19 mwaka huu baada ya kufanyiwa vipimo na baada ya siku 42 tangu kutokea kwa tukio hilo kwa sasa Kagera na Tanzania kwa ujumla ipo salama kwa mujibu wa sheria za afya ulimwenguni.
Naye Katibu Tawala, Mkoa wa Kagera, Toba Nguvila alianza kwa kumshukuru Rais Samia na Waziri huyo wa Afya kwa ushupavu wao katika utendaji kazi kwa kuwapigania Watanzania na kuiomba Wizara ya Afya kujenga Hospitali maalum ya kuhudumia wagonjwa wa magonjwa hatari ya mlipuko, Kituo maalum cha kuratibu magonjwa hayo, kuwapo kwa idara ya afya katika mipaka ya Mkoa huo na nchi jirani, Upanuzi wa Hospitali ya Rufaa na chuo cha Afya Kagemu, Wataalam 48 wa magonjwa ya mlipuko kuendelea kujengewa uwezo wa kitaaluma.
Hata hivyo tukio hilo liliwakutanisha pamoja Viongozi mbalimbali wakiwemo, Wakuu wa Wilaya, Wabunge, Wawakilishi wa Wizara na taasisi mbalimbali, madiwani, vyombo vya ulinzi na usalama na madaktari wa ndani na nje ya Tanzania.
0 Comments