Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Serikali itaendelea kuboresha mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi na Sekondari Tanzania yaani UMITASHUMTA na UMISSETA na kuyafanya kuwa kisima cha wanamichezo mahiri wa Taifa.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA kitaifa yanayofanyika katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Mkoani Tabora.
Ameeleza kwamba Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuunga mkono wanamichezo na kuzipa kipaumbele sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ili ziweze kufaidisha vijana wengi zaidi.
Pia amesema kupitia michezo serikali itaendelea kutoa fursa kwa wanamichezo wanaofanya vizuri zaidi kushiriki katika mashindano ya kimataifa ili kuendelea kuwajengea uzoefu.
Makamu wa Rais Dkt. Mpango ametoa wito kwa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuhakikisha kila shule ya Msingi na Sekondari ina mwalimu wa michezo walau mmoja ili kuweza kuimarisha michezo shuleni na kuwezesha somo la michezo kufundishwa kitaalamu.
Pia amewataka kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya michezo yanalindwa, na kutobadilishiwa matumizi.
Aidha amesema ujenzi wa shule mpya unapaswa kuwa na maeneo ya kutosha kwa ajili ya viwanja vya michezo na upandaji miti.
Hali kadhalika Makamu wa Rais amewasihi wasimamizi wa elimu katika ngazi zote nchini kuzingatia ratiba ya michezo shuleni ili kuwapa wanafunzi muda stahiki kushiriki katika michezo hali itakayopelekea kuibua na kuendeleza vipaji vyao.
Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa Wizara ya Michezo kuangalia namna ya kushirikiana na wadau wengine wa michezo kubuni na kuandaa mipango ya kuwaendeleza vijana wenye vipaji katika michezo na pia kuwapa motisha wanafunzi wanaoshiriki na kufanya vizuri katika michezo.
Amesema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashiriki kwa kushirikiana na Wizara ya Michezo zinapaswa kutafuta fursa mbalimbali za ufadhili ili kuwezesha wanafunzi kubadilishana uzoefu (exchange programs) na kunolewa zaidi katika vilabu mashuhuri vya michezo duniani au kutoka kwa wataalamu wa kimataifa katika fani mbalimbali za michezo.
Kwa upande wake Waziri Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Angellah Kairuki amesema Wizara imeendelea kutoa fedha kila mwaka kwaajili ya mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA pamoja na kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo kwaajili ya shule za msingi na sekondari.
Mhe. Kairuki amesema mashindano hayo yameweka mchango na alama kwa kutoa wachezaji katika timu ya taifa na ambao wameendelea kuiwakilisha vema nchi katika mashindano ya kimataifa.
Ameongeza kwamba zaidi ya asilimia 80 ya wachezaji katika timu za taifa za vijana kama Serengeti Boys, Serengeti Girls na Ngongoro Heroes wametokana na mashindano hayo.
Awali akitoa taarifa ya mashindano hayo, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Dkt. Charles Msonde amesema lengo kuu la Mashindano hayo ni kukuza vipaji vya michezo na taaluma za wanafunzi.
Ameongeza kwamba uendelezaji wa UMITASHUMTA na UMISSETA unatekeleza azma ya serikali ya kukuza sekta ya michezo kwa kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji pamoja na kujenga umoja wa kitaifa, upendo na mshikamano.
Ametaja faida za michezo hiyo ikiwemo kuimarisha afya na ukakamavu miongoni mwa washiriki, kubadilishana ujuzi,maarifa na uzoefu katika michezo pamoja na kuimarisha taaluma ya michezo miongoni mwa wanafunzi.
Mashindano ya UMITASHUMTA kwa mwaka 2023 yanahusisha wanamichezo wanafunzi 3,164 huku mashindano ya UMISSETA kwa mwaka 2023 yatahusisha jumla ya wanafunzi wanamichezo 3,360.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwasili katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Mkoani Tabora kwaajili ya Kufungua Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA leo tarehe 06 Juni 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Angellah Kairuki , Naibu Waziri wa Elimu Omary Kipanga, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi. Dkt. Batilda Burian, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Dkt. Charles Msonde na Mbunge wa Urambo Margaret Sitta pamoja na viongozi wengine wakiimba wimbo maalum wa Michezo na Wanafunzi mbalimbali mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Mkoani Tabora kwaajili ya Ufunguzi wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA leo tarehe 06 Juni 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia Viongozi, Wakufunzi, Walimu , Wanafunzi na Wananchi mbalimbali wakati wa Ufunguzi wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA yanayofanyika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Mkoani Tabora tarehe 06 Juni 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akipuliza filimbi kuashiria Ufunguzi rasmi wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA yanayofanyika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Mkoani Tabora tarehe 06 Juni 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimkabidhi Kitabu cha Mwongozo wa Uendeshaji wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Angellah Kairuki mara baada ya kuzindua kitabu hicho wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA yanayofanyika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Mkoani Tabora tarehe 06 Juni 2023.
0 Comments