Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT.MPANGO AAGIZA KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA ALIYEFANYA UBADHIRIFU WAKATI WA UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA YA TABORA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Tabora kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kuhakikisha wanamfikisha katika vyombo vya sheria aliyefanya ubadhirifu wakati wa Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tabora.

Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo mara baada ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tabora inayogharimu shilingi Bilioni 2.8 iliopo katika kata ya Mpela mtaa wa Uledi Manispaa ya Tabora.

Amekemea vikali tabia ya kukiuka taratibu za manunuzi na kuwataka watumishi wa umma kuhakikisha wanazingatia sheria katika taaluma zao.

Makamu wa Rais amesema changamoto zilizojitokeza katika ujenzi wa Hospitali hiyo hazipaswi kujirudia na kumuagiza Mkurugenzi pamoja na uongozi wa mkoa huo kuweka jicho la pekee na kusimamia vema ujenzi wa Hospitali hiyo ili ikamilike kwa wakati.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewakata wananchi kuwa sauti ya kutoa taarifa pale wanapobaini matukio ya wizi wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Amewataka watumishi kutunza miundombinu iliowekwa pamoja na kuwahudumia wakazi wa eneo hilo kwa upendo na kutumia taaluma zao kuokoa Maisha ya wananchi.

Amesema serikali itaendelea kutekeleza kikamilifu Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa yote yalioahidiwa ikiwemo suala la wananchi kupata huduma bora za afya.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekemea vikali vitendo vya mauaji vinavyojitokeza mkoani Tabora na kuwataka wakazi wa mkoa huo kuacha kujichukulia sheria mikononi.

Amewasihi kutumia njia ya mazungumzo kwa kushirikisha wazee pamoja na viongozi wa dini pamoja na kufuata mkondo wa sheria pale panapotokea migogoro katika familia au jamii.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tabora leo tarehe 06 Juni 2023. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Angellah Kairuki na Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Burian.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akikagua maendeleo ya Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tabora wakati wa Uwekaji Jiwe la Msingi katika Hopsitali hiyo leo tarehe 06 Juni 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akipanda mti aina ya Mparachichi katika Hospitali ya Wilaya ya Tabora wakati wa Uwekaji Jiwe la Msingi katika Hopsitali hiyo leo tarehe 06 Juni 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na viongozi pamoja na watumishi mbalimbali mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tabora leo tarehe 06 Juni 2023.

Post a Comment

0 Comments