Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YATOA TAARIFA HALI YA UCHUMI, PATO LA MTU MMOJA MMOJA LAONGEZEKA KWA ASILIMIA 5.0

Na Mwandishi Wetu,

SERIKALI kupitia Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Mwigulu Nchemba ametoa taarifa ya hali ya uchumi wa nchi ambapo amesema kwa hali ilivyo inaendelea kuifanya Tanzani kuwa nchi ya uchumi wa kati ngazi ya chini.

Dk.Mwigulu ametoa hali ya uchumi leo Juni 15, 2023 Bungeni jijini Dodoma wakati akisoma bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2023/2024 ambapo pamoja na mambo mengine ameelezea hali ya uchumi wa nchi.

Akielezea zaidi kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi mwaka 2022 amesema kwa upande wa uchumi wa Dunia taarif ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Aprili 2023 inaonesha kuwa, kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia imepungua kutoka asilimia 6.3 mwaka 2021 hadi asilimia 3.4 mwaka 2022.

Amesema upungufu huo unatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi wa China na India; madhara ya janga la UVIKO-19; vita kati ya Urusi na Ukraine; na sera za kupunguza ukwasi katika chumi za Ulaya ili kukabiliana na mfumuko wa bei.

Aidha, amesema uchumi wa dunia unatarajiwa kupungua zaidi na
kufikia ukuaji wa asilimia 2.8 mwaka 2023 kutokana na kuendelea kwa vita kati ya Urusi na Ukraine, mabadiliko ya Tabia Nchi na Sera za Marekani kuongeza riba.

VIPI KUHUSU UCHUMI WA AFRIKA NA KIKANDA

Dk.Mwigulu amesema ukuaji wa uchumi kwa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ulipungua kufikia wastani wa asilimia 3.9 mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 4.8 mwaka 2021.

Aidha, ukuaji wa Pato la nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ulikua kwa wastani wa asilimia 4.1 ikilinganishwa na ukuaji wa wastani wa asilimia 5.3 mwaka 2021.

"Vile vile, wastani wa ukuaji wa uchumi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulikuwa ni asilimia 5.3 mwaka 2022 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.3 mwaka 2021. Upungufu huo ulitokana na madhara ya vita kati ya Urusi na Ukraine uliyosababisha mfumuko wa bei za nishati ya mafuta na vyakula, " amesema.


UCHUMI WA PATO LA TAIFA.

Akiendelea kutoa taarifa ya hali ya uchumi Dk.Mwigulu amesema uchumi wa Pato la Taifa katika mwak 2022, thamani halisi ya Pato la Taifa kwa bei za mwaka 2015 lilifikia shilingi trilioni 141.9
ikilinganishwa na shilingi trilioni 135.5 mwaka 2021.

Aidha, kiwango halisi cha ukuaji wa pato la Taifa kilifikia asilimia 4.7 mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 4.9 mwaka 2021. Kiwango hicho cha ukuaji kilitokana na: mikakati iliyochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na athari za vita nchini Ukraine;

Uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu, barabara, reli na viwanja vya ndege; kuongezeka kwa uzalishaji wa madini; kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi iliyochachua shughuli za kiuchumi; na kuongezeka kwa shughuli za utalii.

Amefafanua sekta zilizokuwa na viwango vikubwa vya ukuaji kwa mwaka 2022 ni pamoja na: sanaa na burudani (asilimia 19.0); madini (asilimia 10.9); fedha na bima (asilimia 9.2); malazi na huduma ya chakula (asilimia 9.0); na umeme (asilimia 7.6).

Aidha, kutokana na hatua madhubuti zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali thamani ya Pato ghafi la Taifa linatarajiwa kufikia dola za Marekani bilioni 85.42 mwaka 2023/24.

"Mwaka 2022, Pato ghafi la Taifa (kwa bei za mwaka husika) lilikuwa shilingi trilioni 170.3 (sawa na Dola za Marekeni bilioni 77.6) ikilinganishwa na shilingi trilioni 156.4 mwaka 2021 (sawa na Dola za Marekani billioni 69.94)."

Aidha, Dk.Mwigulu amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, idadi ya watu Tanzania Bara ilikuwa 59,851,347 ikilinganishwa na makadirio ya idadi ya watu 57,724,380 mwaka 2021.

Hivyo, Pato la Taifa kwa Mtu (GDP per capita) kwa mwaka 2022 lilikuwa shilingi 2,844,641 ikilinganishwa na shilingi 2,708,999 mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 5.0.

Amesema kiasi hicho ni sawa na dola za Marekani 1,229.1 mwaka 2022 kwa mtu kwa mwaka ikilinganishwa na dola za Marekani 1,173.3 mwaka 2021. "Hali hii inaendelea kuifanya Tanzani kuwa nchi ya uchumi wa kati ngazi ya chini."

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, Bungeni jijini Dodoma, Juni 15, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, akionesha Bajeti kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, wakati akiwasilisha Bajeti hiyo, Bungeni jijini Dodoma, Juni 15, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Post a Comment

0 Comments