Ticker

6/recent/ticker-posts

ICAP YASAIDIA VITUO VYA AFYA MWANZA VIFAA VYA ZAIDI YA MILIONI 314 KUTEKELEZA PROGRAMU YA SKANA ZA ALAMA ZA VIDOLE

NA BALATZAR MASHAKA, MWANZA

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NACP) unatekeleza mfumo wa kusajili watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) kwa kutumia alama za vidole katika vituo vya afya nchini.

Naibu Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la ICAP nchini Tanzania Dr. John Kahemele, amesema leo jijini Mwanza kuwa hatua hiyo ya kipekee inalenga kuimarisha usiri wa taarifa, upatikanaji wa taarifa sahihi na kuboresha utoaji huduma kwa wagonjwa katika maeneo mbalimbali ya huduma za afya.

Amesema katika katika kutekeleza hilo kwa msaada wa kiufundi kutoka Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC) chini ya ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia Mfuko wa Rais wa Dharura wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) limechangia vifaa mbalimbali ikiwemo skana za vidole vya baiometriki 222, kompyuta 113, moderm za intaneti 40, na mifumo ya UPS 113 kwenye vituo vya afya mkoani Mwanza. Vifaa hivi vilivyochangiwa vina thamani ya sh.314,665,408/-.

“ICAP kwa kushirikianana CDC na wadau wengine inafurahi kuwasilisha skana za vidole vya baiometriki kwenye sekta ya huduma za afya,kwani teknolojia hii ina uwezo wa kubadilisha taratibu za utawala na kuboresha hatua za usalama katika vituo vya afya kwa kutumia nguvu ya utambuzi wa baiometriki, mifumo imara ya kompyuta na uunganisho wa intaneti unaoweza kutegemewa,”amesema.

Dr. Kahemele amesema kuwa lengo lao ni kuboresha usahihi wa utambuzi wawagonjwa, kuimarisha usalama wa taarifa,na kuwezesha wataalamu wa afya kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na kwa usahihi.

“ICAP kwa kushirikiana na NACP na Mwanza RCHMT tutaendelea kutoa uangalizi na msaada wa kiufundi endelevu kwa vituo vya afya wakati wa utekelezaji wa mfumo wa skana ya vidole vya baiometriki.Timu yetu ya wataalamu itafanya kazi karibu na watoa huduma za afya ili kuhakikisha utekelezaji mzuri wa teknolojia hii”, aliongeza.

Naibu Mkurugenzi huyo Mkaazi wa ICAP nchini amesema vifaa hivyo vitasambazwa katika vituo vya afya 208 vinavyosimamiwa na shirika hilo katika halmashauri nane za mkoa huo ambapo hatua hiyo ya pekee inalenga kuimarisha usiri,upatikanaji wa taarifa sahihi na kuboresha utoaji huduma kwa wagonjwa wa maeneo mbalimbali ya huduma za afya.

“Ugawaji wa vifaa hivi vilivyotolewa chini ya Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) kupitia Kituo cha Marekani cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC),unaunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha mazingira ya utoaji huduma za afya,” amesema Dr. Kahemele.

Pia ni utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi uliotoa mwongozo wa kuboresha udhibiti wa taarifa za watu wanaoishi na VVU mbali na kurahisisha uhifadhi wa taarifa na utaondoa matumizi ya karatasi kuhifadhi taarifa zao.

Kwa upande wake Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Mwanza, Dr. Pius Masele amesema hali ya maambukizi mkoani humu siyo ya kuridhisha na vifaa hivyo vitasaidia kufuatilia mwenendo wa maambukizi mapya na kufahamu hali ya mahudhurio katika kliniki za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU.

Amesema takwimu za mwaka 2016/17 zinaonyesha ongezeko la maambukizi ya VVU kutoka asilimia 4.2 mwaka 2011/12 hadi kufikia asilimia 7.2 mwaka 2016/17 huku asilimia 40 ya maambukizi mapya yakiwa ni kwa vijana hususani wa kike.

Dr.Masele amesema zinahitajika juhudi za kuongeza uelewa kwa jamii kutambua kuwa Ukimwi bado upo ili watu wachukue tahadhari ya kujilinda na hatua zenyewe ni pamoja na kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na utunzaji wa taarifa na hiyo itasaidia kufahamu hatua zinazochukuliwa zina tija au la.

Mwenyekiti wa Waganga Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mwanza, Dk Charles Mkombe amesema awali kutokana na matumizi ya karatasi kuhifadhi taarifa, baadhi ya taarifa za watu waishio na VVU zilikuwa zinapotea huku akidai vifaa hivyo vitaongeza ufanisi na usalama katika uhifadhi wa taarifa hizo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amelishukuru Shirika la ICAP kwa msaada huo ambao utakwenda kuwa mkombozi katika kupata taarifa sahihi na ufuatiliaji wa matibabu kwa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI mkoani Mwanza.

"Bado vituo vingine vinahitaji msaada kama huu,hivyo ICAP msiishie hapa endeleeni kutupigania wakati huu ambao serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kutoa huduma za afya nchini,”amesema Makilagi.

Pia amewataka wasimamizi wa hospitali na vituo vya afya vitakavyonufaika na vifaa hivyo kuvitunza na kutumika kwa muda mrefu ili vilete tija huku akiiomba ICAP kuendelea kuimarisha mifumo na uboreshaji wa huduma za afya mkoani humu.


Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi (katikati) akikata utepe katika hafla ya kukabidhiwa vifaa ukusanyaji taarifa, usiri wa wateja,usajili na ufuatiliaji wa wateja wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVIU) leo.Vifaa hivyo vimetolewa na Shirika la ICAP Tanzania.
Ofisa Takwimu wa Wilaya ya Ilemela, Nabil Nuru akimwonyesha Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana namna usajili wa Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi unavyofanyika kwa kutumia kompyuta na skana ya vidole, leo.

Naibu Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la ICAP Tanzania, Dr. Johm Kahemele (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, moja ya vifaa vilivyotolewa na shirika kwa ajili ya vituo vya afya vinavyowahudumia watu wanaoishi na Virusi vya ukimwi mkoani Mwanza leo.
Post a Comment

0 Comments