Ticker

6/recent/ticker-posts

KIJIJI CHAVUNA MILIONI 107,115,000 UVUNAJI WA MSITU WA HIFADHI WA KIJIJI.

NA YEREMIAS NGERANGERA…NAMTUMBO

Kijiji cha Kitanda wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma chanufaika na shilingi milioni 107,115,000 kutokana na uvunaji wa msitu wa hifadhi wa kijiji hicho kuanzia mwaka 2021 mpaka mwaka 2023.

Mtendaji wa kijiji cha kitanda Ayubu Muhuwa alisema kijiji cha kitanda kilipata fedha hiyo kutokana na kuvuna msitu wa hifadhi ya kijiji uitwao Mtaungana wenye ukubwa wa hekta 11,930.

Muhuwa alidai kijiji cha Kitanda kilipata elimu ya mradi wa uhifadhi kutoka MJUMITA,WWF na MCID(MPINGO) kuanzia mwaka 2016 na baada ya hapo walitafuta wavunaji wa magogo kutoka kwenye msitu wao na kujipatia shilingi milioni 107,115,000.

Joseph Kanisius Ngonyani mwenyekiti wa kijiji cha Kitanda pamoja na kukiri kupokea kiasi hicho cha fedha alifafanua mgawanyo wa fedha hizo kuwa shilingi 62,126,700 zilipelekwa kwa Halmashauri ya kijiji cha kitanda,shilingi 5,355,750 zilipelekwa kwenye ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo na shilingi 39,632,550 zilipelekwa kwenye kamati ya maliasili kijiji cha kitanda alifafanua mwenyekiti huyo

Ngonyani alidai kuwa, kupitia mapato yaliyotokana na uvunaji wa msitu huo wa hifadhi kijiji kupitia mgao huo wa shilingi 62,126,700 kilitoa fedha kwa kila shule shilingi milioni 1,280,000 kwa shule 3 za msingi ya Lugongoro, Kitanda na shule ya msingi ya Mkomanile zote za kijiji hicho jumla ya shilingi 3,840,000 kwa ajili ya kutengenezea madawati.

Hata hivyo Ngonyani alidai kupitia fedha hizo pia waliweza kutumia kiasi cha 29,939,500 kujenga jengo la huduma ya mama na mtoto (maternity) baada ya kuwa na hitaji hilo kutoka kwenye zahanati yao ya kijiji na kisha kutumia shilingi 21,371,000 kujenga nyumba mbili za waganga jengo ambalo nalo lipo katika hatua ya ukamilishaji.

Afisa misitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Gravas Mwalyombo pamoja na kukipongeza kijiji cha Kitanda kwa kusimamia vyema msitu wa hifadhi ya kijiji, aliwapongeza viongozi na wananchi wa kijiji hicho kwa kutumia pato litokanalo na uvunaji wa misitu kuondoa changamoto zinazowakabili katika kijiji chao.

Mwalyombo alidai maono waliyonayo wananchi na viongozi hao kujenga miundombinu katika kuboresha zahanati yao na kuimarisha elimu kwa kutengeneza madawati ni jambo la kuigwa na viongozi wa vijiji vingine.

Kijiji cha Kitanda ni miongoni mwa vijiji vya wilaya ya Namtumbo venye utajiri mkubwa wa misitu vilivyotengwa na kijiji kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi ambapo kupitia msitu huo waliweza kuvuna magogo yenye jumla ya meta za ujazo (CBM) 369.362. na kuuza na kukipatia shilingi 107,115,000.


Post a Comment

0 Comments