Na Said Mwishehe,
LIONS Club Dar es Salaam imeweka kambi maalum ya kufanya uchunguzi wa macho kwa wazee wa mkoa huo ambapo wazee 1470 wamefanyiwa uchunguzi huo na kati yao 168 wamebainika wanahitajika kufanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho.
Miongoni mwa wazee hao wapo wanaoishi katika kambi ya wazee wasiojiweza iliyopo Msimbazi Centre jijini Dar es Salaam huku ikielezwa kuwa uchunguzi na mabatibabu yote yametolewa bure kwa wazee hao.
Akizungumza na Michuzi TV na Michuzi Blog leo Julai 16,2023 jijini Dar es Salaam wakati wa kambi hiyo Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho Majala Majala amesema Lions Club ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na washirika wake wameona kuna haja ya kuwafanyia uchunguzi wazee wa Dar es Salaam wanaolelewa kwenye kambi hiyo pamoja na wazee wengine.
“Jana Julai 15,2023 tumefanya uchunguzi kwa wagonjwa zaidi ya 1,470 na tukapata wagonjwa 168 ambao watahitaji kufanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho na leo tumeanza kufanya upasuaji kuondoa mtoto wa jicho kwa wazee hao.Wengine wamepewa miwani na dawa bure.”
Alipoulizwa mtoto wa jicho ni nini, amejibu ni lensi ya jicho ambayo inatakiwa kuwa safi na inapaswa kuonekana kama kioo cha mbele ya gari , kwa hiyo kadri mtu anavyokuwa kuna mabadiliko kwenye mwili wake yanatokea , miongoni mwa viungo ambavyo vinapata mabadiliko ni pamoja na lensi ya jicho ambayo inapata rangi ya maziwa maziwa na hatimaye inaziba kabisa
“Ndio maana mtu anakwambia ninaona ukungu sasa ule ukungu ndio lensi inaanza kuwa na rangi ya maziwa maziwa na hivyo lensi inafunga,”amesema huku akisisitiza sababu za mtoto wa jicho ni umri unavyoongezeka ndivyo inavyokuwa rahisi kupata.
Pia amesema wapo wengine wanapata mtoto wa jicho kutokana na matumizi mabaya ya dawa, lakini wengine wanapata kutokana na kuumia huku wengine wanaweza kupata mtoto wa jicho kutokana na maradhi ya sukari na presha waliyonayo.
“Kwa wale wa umri mkubwa ni ngumu kuepuka, lakini kwa wale wanaotumia dawa inawezekana, wagonjwa wa sukari na presha wanatakiwa kushiriki kwenye kliniki zao vizuri ili kudhibiti sukari na presha,”amesema Dk.Majala
Alipoulizsa kuhusu kasi ya mtoto wa jicho amefafanua sio ugonjwa wa kuambukiza, hivyo kadri watu wanavyokuwa na umri mkubwa ndivyo inakuwa rahisi kupata mtoto wa jicho.
“Tuliwahudumia kwenye kambi yetu kuna wenye umri kuanzia miaka 50 na mwenye umri mkubwa zaidi alikuwa ni umri wa miaka miaka 105.”
Kwa upande wake Mwenyekiti Mstaafu wa Lions Club kitaifa Mustanzil Gulahusein amesema mtoto wa jicho mara nyingi hutokea kwa watu wenye umri mkubwa huku akiwasihi wananchi wajitokeze kwa wingi kuwasaidia hao wazee kwani kuwarudisha macho ni sawa na kumrudishia uhai.
“Wakiwa na macho ambayo hayana changamoto yoyote wanaweza kushughulika na kilimo au kazi ndogo ndogo kwa ajili ya familia.Wazee wakiwa na tatizo la macho maana yake kuna mtu mwingine atakuwa anasimamia .”
Kuhusu kambi ya macho, amesema wamekuwa wakifanya katika maeneo mbalimbali zaidi ya Dar es Salaam na mikoani hasa maeneo ya vijijini na siku za karibu wametoa huduma kama hiyo Handeni mkoani Tanga.
Pia kambi kama hiyo walifanya pia Kahama na Nyamagana huku akifafanua mwaka jana wamefanya upasuaji wa macho kwa zaidi ya 2000 na mwaka huu kuanzia Julai hadi sasa wamefanyia upasuaji watu 400.
Ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa Lions Club wamekuwa na utaratibu wa kusaidia jamii hasa katika kufanya uchunguzi wa macho na kutoa matibabu ya dawa pamoja na upasuaji huku akitoa mwito jamii ifanye jitihada za kusafisha macho na watu wenye umri mkubwa wawe wanafanya uchunguzi wa macho mara kwa mara ili kama kuna tatizo liweze kutatuliwa mapema.
Matukio mbalimbali wakati wa kambi ya uchunguzi wa macho ikiendelea katika kambi ya wazee wasiojiweza jijini Dar es Salaam
0 Comments