Ticker

6/recent/ticker-posts

MHE.HEMED SULEIMAN ASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA IDADI YA WATU DUNIA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kusimamia Sera na mikakati mbali mbali katika kuhakikisha inawawekea wananchi wake mazingira bora na ya usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa uzazi salama na kutanua fursa kwa wanawake na wasichana.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa Kauli hiyo katika Maadhimisho ya siku ya Idadi ya watu Dunia Kitaifa iliyofanyika ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein Tunguu Mkoa wa kusini unguja.

Amesema Serikali zote mbili zimekuwa zikisimamia Sera na mikakati hiyo kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 - 2025 ambapo katika utekelezaji wa hatua hizi imechukua hatua mbali mbali zikiwemo kuongeza Idadi ya wanawake katika ngazi mbali mbali za Uongozi ikiwemo Baraza la Wawakilishi, Bunge na Mawizara hatua ambayo inatoa fursa kwa wanawake kutumia ujuzi, maarifa na elimu zao katika kuisaidia Serikali kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

Amesema Serikali imeamua kuanzisha Wizara maalumu inayoshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa SMZ na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa SJMT ili kuhakikisha ustawi unaimarila hasa kusimamia hadhi na mchango wa wanawake na Makundi Maalumu nchini.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeweka mazingira bora ya kusomeshea na kujifunzia kwa kujenga skuli Tisa (09) za ghorofa katika ngazi ya Msingi na Sekondari kwa Unguja na Pemba pamoja na ujenzi wa Dakhalia za wasichana katika Skuli mbali mbali ikiwemo, Lumumba, Paje - Mtule na Ujenzi wa Dakhalia ya wasichana Katika Skuli ya Chwaka Tumbe inayotarajiwa kuanza hivi karibuni kwa upande wa Pemba.

Akizungumzia suala la Uwezeshaji uzazi salama Mhe. Hemed amesema Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbali mbali wa Maendeleo imeweza kupunguza Idadi ya Vifo vya Mama na watoto wa wachanga ambapo katika kufikia malengo hayo imehakikisha Vituo vya Afya na Hospitali zote nchini zina miundombinu Mizuri pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba vya Mama na mtoto.

Aidha Mhe. Hemed amezishukuru Serikali za Mikoa na Wilaya Nchini kwa kuhakikisha inasimamia kwa dhati zoezi la Sensa ya Watu na Makazi nchini iliyofanyika mwezi Agosti mwaka jana hatua ambayo imesaidia kupata Idadi sahihi ya wananchi wanaoishi Tanzania hatua ambayo itaisaidia Serikali kuweza kupanga mipango endelevu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikagua Mabanda ya Maonesho ya Taasisi za Umma na Binafsi katika Maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani iliyofanyika ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein Tunguu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman akiwahutubia viongozi na wananchi mbali mbali katika ukumbi wa Mkutano wa Dkt. Ali Mohammed Shein Tunguu alipohudhuria katika maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Dunia.

Post a Comment

0 Comments