Ticker

6/recent/ticker-posts

TANZANIA, HUNGARY WAKUBALIANA KUSHIRIKIANA, KUBADILISHANA WANAFUNZI ELIMU YA JUU

Na Said Mwishehe

RAIS wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ametangaza makubaliano ya ushirikiano katika maeneo mbalimbali yaliyofikiwa kati ya Tanzania na nchi ya Hungary.

Katika makubaliano hayo miongoni mwa mambo waliyokubaliana ni pamoja na kuendelea kubadilishana wanafunzi wa elimu ya juu hasa katika eneo la sayansi, tekonolojia, uhandisi na hisabati.

Makubaliano hayo yametangazwa leo Julai 18 Ikulu jijini Dar es Salaam na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa upande na Tanzania na Rais Katalin Novak wa Hungary ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi ya siku nne na aliwasili nchini Julai 17 na anatarajiwa kuondoka Julai 20 mwaka huu.

Akizungumza kuhusu ziara ya Rais Novak, Rais Dk.Samia ameeleza nchi hizo mbili zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu katika eneo la elimu uwekezaji na biashara.

Rais Samia amesema utiaji saini uliofanyika kati ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania Prof. Adolf Mkenda na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kutoka Hungary Tristan Azbej unaenda kufungua ukurasa mpya kwa nchi hizo kwenye sekta husika.

"Kwa miaka mingi nchi hii imekuwa ikifadhili wanafunzi wa Tanzania kwenda masomo katika ngazi ya shahada ya kwanza, uzamili na uzamivu, hivyo katika kuhakikisha wanaunga mkono juhudi hizo Tanzania itakuwa inatoa ufadhili kwa wanafunzi 30 kutoka Hungary kuja kusoma masomo ya elimu ya juu, " amesema Rais Samia

Pamoja na hayo Rais Samia amesema katika mazungumzo waliyoyafanya wamekubaliana pia umuhimu wa kuanzisha mashauriano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Hungary huku akifafanua hiyo itawezesha Serikali zao kushirikiana na kufanya mashauriano kwenye maeneo yenye maslahi waliyokubaliana.

"Pia tumekubaliana kushirikiana kuhamasisha wawekezaji kwenye sekta ya utalii inayoendelea kukuwa kwa kasi.Takwimu zinaonesha watalii zaidi ya 70,000 wametembelea nchini...nikuombe Rais Katalin Novak ukawe balozi mzuri kuvitangaza vivutio vya utalii, " amesema.

Rais Samia amemueleza Rais Novak kwamba nchi ya Tanzania imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii,hivyo ukirudi nyumbani akawe balozi wa kutangaza vivutio hivyo.

Kwa upande wake Rais Katalin akizungumza kuhusu makubaliano waliyoingia amesema Tanzania ni moja ya nchi ambayo idadi ya watu inaongezeka kwa kasi hivyo ni muhimu kuweka mkazo katika elimu ili kuendelea kutatua changamoto zilizopo

Pia amesema wamekubaliana kila upande wataendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 200 ambao watataka kusoma nchini Hungary na katika suala la usawa wa kijinsi na uwezeshaji wanawake kiuchumi ni jambo ambalo wataliwekea mkazo.

Ameongeza wanapaswa kuwekeza kwa wasichana ili washiriki kwenye uongozi na wafikie ambako wao wamefika akitolea mfano yeye na Dk. Samia kuwa marais.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mgeni wake Rais wa Hungary Mhe. Katalin Novák wakishuhudia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolph Mkenda pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kutoka Hungary Tristan Azbej aliyeiwakilisha Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Nchi hiyo wakati wakisaini Hati ya Makubaliano baina ya nchi mbili kuhusu Ushirikiano wa ndani wa Programu ya Stipendium Hingaricum ya mwaka 2024-2026, Ikulu Jijini Dar es Salaam. Stipendium Hingaricum ni Programu ya ufadhili wa masomo ya Elimu ya Juu (Scholarship) inayotolewa na Serikali ya Hungary kwa ajili ya Wanafunzi wa kigeni.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kutoka Hungary Tristan Azbej aliyeiwakilisha Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Nchi hiyo wakati wakisaini Hati ya Makubaliano baina ya nchi mbili kuhusu Ushirikiano wa ndani wa Programu ya Stipendium Hingaricum ya mwaka 2024-2026, Ikulu Jijini Dar es Salaam. Stipendium Hingaricum ni Programu ya ufadhili wa masomo ya Elimu ya Juu (Scholarship) inayotolewa na Serikali ya Hungary kwa ajili ya Wanafunzi wa kigeni.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mgeni wake Rais wa Hungary Mhe. Katalin Novák wakati wakizungumza na Waandishi wa Habari Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Julai, 2023. Rais Novák yupo nchini Tanzania kwa ziara ya siku tatu.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waandishi wa Habari Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Julai, 2023 wakati wa ziara ya Rais wa Hungary Mhe. Katalin Novák nchini. Rais Novák yupo nchini Tanzania kwa ziara ya siku tatu.
Rais wa Hungary Mhe. Katalin Novák akizungumza na Waandishi wa Habari Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Julai, 2023.

Viongozi mbalimbali pamoja na Waandishi wa Habari waliohudhuria Mkutano wa Wanahabari kuhusiana na Ziara ya Rais wa Hungary Mhe. Katalin Novák Ikulu Jijini Dar es Salaa.

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)




Post a Comment

0 Comments