Ticker

6/recent/ticker-posts

WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI WAASWA KUZINGATIA SHERIA ZA MADINI KUPUNGUZA MIGOGORO - NYAMONGO


Na Mwanahamisi Msangi, Mara

Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Henry Mditi amewaasa Wachimbaji na Wafanyabiashara wa Madini Nchini kuzingatia Sheria, Usalama, Utunzaji wa Mazingira na Matumizi salama ya baruti katika uendeshaji wa shughuli za uchimbaji madini ili kupunguza migogoro isiyokuwa na tija migodini.

Mhandisi Mditi ameyasema hayo leo Julai 21, 2023 kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba kwenye ufunguzi wa mafunzo ya Usalama, Afya,Utunzaji wa Mazingira na matumizi salama ya baruti kwa wachimbaji wadogo wa madini, yaliyofanyika Wilayani Tarime mkoani Mara ambayo yameshirikisha pia Wakurugenzi, Mameneja, Watumishi kutoka Tume ya Madini, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Viongozi wa Wachimbaji Wadogo na Wachenjuaji wa Madini pamoja na Wafanyabiashara na wamiliki wa migodi wa eneo la Nyamongo.

Mhandisi Mditi amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha kuwa shughuli za uchimbaji na uchenjuaji, na biashara ya madini zinafanyika kwa kuzingatia Usalama, Afya na Utunzaji wa mazingira kwa kufuata Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali iliyowekwa.

“Tunatambua kwamba shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini zina manufaa mbalimbali kwa mchimbaji, wananchi na Taifa kwa ujumla kupitia fursa za ajira, biashara na mapato mbalimbali kwa serikali,” amesema Mhandisi Mditi.

Amesema kuwa mafunzo hayo yameangazia pia utaratibu wa utoaji leseni za uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini hususan kwenye usimamizi wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini.

" Ni muhimu shughuli hizo kufanyika kwa kuzingatia Usalama, Afya na Utunzaji wa mazingira ili kuzifanya kuwa endelevu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo, hivyo mafunzo haya yatiliwe mkazo namna ya kuepuka na ajali migodini, utunzaji wa mazingira, afya na matumizi sahihi ya baruti." amesema Mhandisi Mditi.

Ameongeza kuwa, “Kupitia mafunzo haya naamini mna wajibu mkubwa wa kuimarisha mfumo wenu wa utendaji kazi kwa kuangalia usalama katika maeneo mnayochimba ili kuhakikisha kuwa taifa halipotezi nguvu kazi ili tuwe na uchimbaji endelevu wa kuimarisha maisha yetu na jamii inayotuzunguka,"

Wachimbaji wa madini 105 kutoka eneo la Nyamongo Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara wameshiriki mafunzo hayo ya siku moja ambapo, wametakiwa kuepuka utoroshaji wa madini kwani kwa kufanya hivyo watasababisha Serikali kukosa mapato na kushindwa kutoa huduma za msingi za kijamii zenye tija ikiwemo elimu bure na afya.

Post a Comment

0 Comments