Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI DKT. ASHATU KIJAJI ASISITIZA USIMAMIZI WA USAHIHI WA VIPIMO AKIZINDUA BODI MPYA YA USHAURI WMA

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) asisitiza bodi mpya ya ushauri ya Wakala wa Vipimo kuhakikisha walaji wanalindwa kupitia uhakiki wa vipimo ili wanaponunua bidhaa mbalimbali wapate kuona thamani ya fedha katika bidhaa wanazonunua.

Dkt.Kijaji ameyasema hayo Jijini Dodoma leo tarehe 27 Julai, 2023 alipokuwa anazindua bodi ya sita ya ushauri ya Wakala wa Vipimo.

Aidha, amemshukuru Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala pamoja na wajumbe kwa kuaminiwa na kuteuliwa kwani wanaunda timu bora na inayotoa matumaini makubwa katika kuendelea kusimamia matumizi sahihi ya Vipimo kwenye bidhaa pamoja na vifungashio vyake ili watumiaji waweze kupata kile walichokilipia. 

Pia, ameitaka bodi kufanya kazi yake kwa weledi na kuhakikisha inasimamia usalama wa mali za watanzania kupitia vipimo sahihi ambapo matarajio ya Serikali ni kwamba wataisaidia wakala katika kuhakikisha inatekeleza vipaumbele vya serikali kwenye usimamizi wa matumizi sahihi ya vipimo nchini, na kupitia usimamizi huo wataweza kuwahudumia wafanyabiashara na wawekezaji na kuishauri serikali kuhusu masuala yote yanayohusu vipimo na kuhakikisha wakala inamlinda mlaji kwa kutumia vipimo sahihi Dkt. Kijaji amesema.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Kijaji ameitaka wakala kuwa pamoja na kazi nzuri wanayoifanya ya usimamizi wa vipimo ni vyema kuendelea kuongeza nguvu katika kusimamia usahihi wa vipimo kwenye maeneo mbalimbali

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Vipimo, Dkt. Eliza Alfred Mwakasangula alimshukuru Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), pamoja na Menejimenti ya Wakala kwa kuahidi kusimamia na kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na kushauri Wizara ipasavyo kwenye masuala ya vipimo ili kuhakikisha wakala inaendelea kutoa huduma bora kwa Wananchi inao wahudumia.

Wakati huohuo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Bi. Stella Kahwa amemshukuru Waziri kwa kuteua Bodi ambayo itasaidia kuleta maendeleo kwa wakala, ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya vipimo vinavyohakikiwa kwa mwaka na kuhakikisha Wakala inaendelea kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments