Ticker

6/recent/ticker-posts

MAJALIWA ATILIA MKAZO KIPAUMBELE KWA MWANAMKE KATIKA FURSA.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima akiongea na wanawake mkoani Tanga kabla ya kufunga kongamano lao.
Mbunge Ulenge akiongea na wanawake.


Baadhi ya wanawake walioshiriki kwenye kongamano.


Waziri Dkt. Gwajima wa kwanza kulia akisalimiana na mbunge viti maalumu Mkoa wa Tanga Mwanaisha Ulenge alipoingia ukumbi wa Legal Naivera, wa kwanza kushoto ni mbunge wa Tanga, na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu.




*********************

Na Hamida Kamchalla, TANGA.


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesisitiza kwa wenye makampuni na taasisi k utoa kipaumbele cha ajira kwa wanawake, ikiwa ni pamoja na fursa za biashara na manunuzi ya umma katika miradi yote ya kimkakati inayotekelezwa nchini kwa kuzingatia ujuzi wao lakini pia bidhaa walizonazo.


Ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi wakati wa ufungaji wa kongamano la wanawake na manunuzi ya umma, fursa za biashara katika mradi wa bomba la mafuta Mkoa wa Tanga ambapo aliwakilishwa na Waziri wa Maendeleo yaJamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima.


Aidha Majaliwa amesisitiza kwamba ufuatiliaji na tathimini ufanye katika miradi ya kimkakati juu ya Watanzania uendelee kufanyika na taarifa ziwe zinatolewa ili serikali iweze kuchukua hatua stahiki katika kukabiliana na matatizo yanayojitokeza mara kwa mara ili ushiriki wao uwe na manufaa kwao na Taifa kwa ujumla.


"Taarifa zote kupitia kwenye mradi ziangalie uwiano wa kijinsia ili kutekeleza azma ya Mh. Rais Samia Suluhu Hassan, ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, hivyo wadau wajue tukifuatilia hizi taarifa kuwa ni maelekezo ya mamlaka" amesema.


"Lakini wawekezaji na wakandarasi wa Kimataifa wahakikishe kuwa masuala ya kujenga ujuzi kwa Watanzania, uhaulishaji wa tekinolojia na ushiriki wa jamii kwenye eneo la uwekezaji yanapewa kipaumbele" amefafanua.


Vilevile amebainisha kwamba taasisi zote zinazotekeleza au kusimamia miradi ya kimkakati, wawakilishe taarifa za utekelezaji wa ushiriki wa Watanzania kwenye miradi hiyo na uwekezaji kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji ili kuwezesha nchi kupima thamani inayobaki kwenye uchumi wa nchi kutokana na ushiriki wa Watanzania.


"Na hapa niwakumbushe ninyi, mna majukwaa ya wanawake, Dkt.Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuyaimarisha kwelikweli na huko kwenye hayo majukwaa ndiko hivi vitu vingine baada ya makongamano haya vitakuwa vikisemwa, ili hata haya tunayoagiza hapa muende kunyanyua hoja kwamaana hizi pia ni ajenda mtakazojadiiana kwenye majukwaa yenu" amesisitiza.


Hata hivyo amezitaka taasisi za fedha pia kutoa mikopo kwa wanawake wenye kukidhi vigezo ili kuwapatia mitaji na elimu ya masuala ya fedha ili waweze kushiriki vema kwenye manunuzi ya umma pamoja na fursa nyingine kwenye mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta na miradi mingine ya kimkakati.


"Wadau wa maendeleo, taasisi na mashirika wasaidiane na serikali kuwajengea uwezo ili waweze kuwa na ujuzi wa kuwajibika kuzalisha bidhaa zenye viwango vya kiushindani na kutoa huduma bora kwa wawekezaji na wakandarasi katika miradi ya kimkakati" amesema.


Naye Mkurugenzi wa Unganisha Maisha Foundation, Mwanaisha Ulenge ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Tanga amesema alianzisha taasisi hiyo isiyo ya kiserikali mwaka 2021 kwa mujibu wa sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali, imelenga kutoa mafunzo na kumuwezesha mwanamke kushiriki katika manunuzi ya umma, kupata fursa na biashara kwenye mradi wa bomba la mafuta.


Ulenge amefafanua kwamba taasisi hiyo haitasita kutoa mafunzo ya aina hiyo mahali popote mbali ya Mkoa wa Tanga kwani imedhamiria kuunga mkono kikamilifu juhudi za serikali katika utekelezaji wa mipango yake.


"Taasisi inatambua juhudi kubwa zinazofanywa na serikali kupitia sekta mbalimbali ili kumuwezesha Mtanzania kuwa na maendeleo endelevu, pia nimedhamiria kujikita katika makundi maalumu, wakiwamo wanawake kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi kuwa endelevu, na nitahakikisha kuwa hakuna anayeachwa nyuma" amesema.


"Katika kutekeleza malengo niliyojiwejea, nitahakikisha fursa mbalimbali zinazotokana na utekelezaji wa mipango ya serikali zinawafikia walengwa, wakiwamo wanawake, ili dhamira yangu ya kusaidia iweze kukidhi nimeona ni vema nikianzisha taasisi hii ili nipate fursa ya kuisaidia jamii kwa upana zaidi" amefafanua.

Post a Comment

0 Comments