Ticker

6/recent/ticker-posts

MKONGE KUBADILI MAISHA WA KULIMA WA ZAO HILO, DC MWEGELO AFAFANUA*************

Na Hamida Kamchalla, KOROGWE.


MKUU wa Wilaya ya Korogwe, Jokate Mwegelo amesema kwa kipindi chote atakachokuwa wilayani hapo, atakuwa Balozi wa zao la Mkonge kwa kuwa ndiyo zao linalokwenda kubadili maisha ya watu.

Jokate ameyasema hayo wakati akizindua jengo la ofisi ya Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) cha Magoma wilayani Korogwe mkoani Tanga, ambacho kiameandika historia ya kuwa Amcos ya kwanza ya Mkonge kuwa na ofisi yake.


“Niwapongeze Amcos ya Magunga kwa hatua ya kuwa na ofisi yenu wenyewe. Tanzania ina vyama vya ushirika 6,000 lakini kwenye Mkonge ninyi ndiyo wa kwanza kuwa na ofisi yenu,


“Nimesema nitakuwa Balozi wa Mkonge kwa kipindi nitakachokuwa Korogwe kwani ninafahamu jinsi gani hili zao linakwenda kubadilisha maisha ya watu, tulikuwa wazalishaji kinara duniani, historia hiyo njema inakwenda kujirudia chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa sababu serikali iko bega kwa bega na wakulima wa Mkonge hadi kieleweke" amesema.


Aidha, ameitaka Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) na wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana na kuziunga mkono Amcos kutimiza malengo ambayo wamejiwekea kama ilivyokuwa kwa Magoma.


Pamoja na hayo, Mwegelo amesema serikali imekataza matumizi ya vifungashio na kamba za plastiki kwa sababu matumizi yake yanasababisha uchafuzi wa mazingira ambapo ili kukabiliana na hayo mbadala wake ni Mkonge.


“Tukatae matumizi ya mifuko ya plastiki, mwelekeo wa dunia ni kutunza na kulinda mazingira, hii ni fursa na ambao watanufaika nayo ni ninyi wazalishaji wa Mkonge" amesema.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona amesema uzalishaji Mkonge nchini kwa asilimia kubwa unategemea Mkoa wa Tanga hasa Wilaya ya Korogwe ambapo kwa kipindi cha mwaka 2022 uzalishaji Mkonge ulikuwa tani 48,000 Mkoa wa Tanga ukichangia tani 33,000, Wilaya ya Korogwe tani 14,000 na katika tani hizo 14,000 wakulima wadogo wamechangia tani 7,000.


“Uzalishaji uliongezeka zaidi baada ya ujio wa Kampuni ya Sisalana lakini tuliona ni vyema tukatoa vibali ili kila Amcos imiliki kiwanda cha uchakataji kwa kuwa na korona yake kwa sababu malalamiko ya wakulima yalikuwa mengi.


“Kwa hiyo kwa kuwaruhusu kuwa na korona moja haimaanishi tunataka kuiondoa Sisalana bali kuitia shime kwani tuna muda mfupi kutimiza lile lengo la Ilani ya Uchaguzi kuzalisha tani 80,000 mwaka 2025 na lile la serikali kuzalisha tani 120,000 ifikapo mwaka 2025/26,


"Na ili tuwezi kufikia malengo hayo kama hatufanyi chochote huku chini, tuliona ni wakati muafaka tuwape nafasi Amcos nao waongeze korona ili tuongeze uzalishaji,” amesema.


Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sisalana, Elizabeth Kalambo aliipongeza Amcos hiyo kwa kushirikiana vizuri na kujituma kwao ndiyo wamefanikiwa kujenga jengo lao ndani ya muda mfupi.


Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Tanga, John Henjewele amesema; “Naipongeza TSB kwa kuona umuhimu wa kuwapatia Amcos maeneo ambapo leo hii tunashuhudia utekelezaji umezaa matunda, naiomba TSB iendelee kushirikiana na vyama vingine.”


Meneja wa Amcos ya Magoma, Maneno Jackson amesema ujenzi wa ofisi hiyo umegharimu Sh milioni 72, na imejengwa kwa miaka mitatu tangu mwaka 2020 na kukamilika mwaka huu 2023.

Post a Comment

0 Comments