*Rais aipa kongole TCRA kwa ushiriki wake kama mbia wa mradi
Na Mwandishi Wetu Arusha,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua jengo refu zaidi jijini Arusha, ambalo sasa ni Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU).
Katika hafla hiyo muhimu, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa jengo hilo katika kukuza sekta ya posta barani Afrika, akisema ni tukio la kihistoria kwa Afrika. Alitumia fursa hiyo kuipongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na PAPU kwa ushirikiano wao imara uliosaidia kufanikisha mradi huu wa kuvutia.
"Nawapongeza sana TCRA na PAPU kwa kukamilisha mradi huu mkubwa," Rais Samia alisema. "Jengo hili litasaidia kukuza sekta ya posta barani Afrika na kuboresha huduma kwa wananchi."
Jengo la PAPU Tower lina ghorofa 17, limegharimu Billion shilingi bilioni 54.86. ambapo asilimia 60 ya gharama hizi zimetolewa na PAPU, huku asilimia 40 nyingine zikitolewa na TCRA kama mbia wa mradi kwa niaba ya Serikali ya Tanzania.
Katika hafla hiyo ya kihistoria, Rais Samia pia alizindua stempu mbalimbali zilizotolewa na Mashirika ya Posta wanachama wa PAPU, ambazo zinaonesha picha ya jengo hili lenye muonekano wa kipekee ambazo zitatumiwa kote Duniani katika shughuli za kila siku za kiposta.
Jengo la PAPU Tower lilianza kujengwa mwaka 2019 na kukamilika mwaka 2023. Ujenzi wa jengo hilo ulisimamiwa na kampuni ya ujenzi ya China State Construction Engineering Corporation, huku Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ikisimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ambao umependezesha mandhari ya jiji la Arusha.
Kabla ya tarehe ya uzinduzi, kulifanyika mikutano muhimu kujadili na kuweka mikakati ya kufanikisha mradi huu wa kuvutia na kuboresha sekta ya Posta Afrika. Mikutano hii ilihudhuriwa na viongozi na wanachama wa PAPU, Serikali ya Tanzania, pamoja na Mkutano wa Mawaziri wa Sekta ya Posta na Watendaji Wakuu wa Mamlaka za Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano. Walijadili namna nchi wanachama zinavyoweza kuondoa vikwazo vinavyosababisha kusuasua kwa ukuaji wa haraka wa sekta ya Posta barani Afrika.
Uzinduzi wa jengo la PAPU Tower unaashiria ushirikiano na maendeleo katika eneo la posta barani Afrika. "Jengo hili litasaidia kuboresha huduma za posta kwa wananchi wa Afrika na litaimarisha ushirikiano wa kimataifa, huku Tanzania ikiendelea kujijengea sifa ya kimataifa," alieleza Oyuke Phoustine, Afisa Habari wa PAPU.




0 Comments