Ticker

6/recent/ticker-posts

HISTORIA YA VIONGOZI WA MAHAKAMA KUANDIKWA, IKIWEPO YA JAJI KISANGA.


*************

Na Hamida Kamchalla, LUSHOTO.

JAJI Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma amekitaka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kuendeleza utamaduni wa kuandika historia za viongozi waliopita hatua itakayosaidia kuhifadhi na kuonyesha michango yao katika kutumikia Mhimili wa Mahakama.

Jaji Mkuu ametoa kauli hiyo Novemba 24,2023 katika hotuba yake aliyoitoa alipokuwa mgeni rasmi katika Mahafali ya 23 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ambapo jumla ya wanachuo 851 wamehitimu Kozi ya Sheria kwa ngazi mbalimbali.

Alisema Chuo cha Uongozi wa Mahakama kimejiongezea majukumu na kujipambanua kwenye eneo la uchapishaji wa vitabu ikiwemo kile kinachoelezea Maisha na Ndoto ya Marehemu Jaji wa Mahakama ya Rufaa Robert Habesh Kisanga kinachoitwa A Dream Coming to Fruition: A Biography of Justice Robert Habesh Kisanga.

Alisema kuwa zoezi walilokamilisha la uandishi wa Kitabu kinachoelezea historia ya Jaji Kisanga ni kazi nzuri ambayo inapaswa kuendelezwa kuandika katika Historia za Viongozi wengine wa Mahakama ya Tanzania wakiwemo Majaji na Mahakimu ambao katika utekelezaji majukumu yao wamefanya makubwa ambayo yanapaswa kukumbukwa daima.

Prof. Juma alisema machapisho mengine yanayopaswa kufanyiwa kazi ni Utafiti wa utamaduni wa kimahakama (Exploring Judicial Culture in Tanzania) na mkusanyiko wa kesi za unyanyasaji wa kingono kwa watoto kwa nchini Tanzania pamoja na Ireland (A Compendium of Child Sexual Abuse Cases of Tanzania and Ireland)

Wakati huo huo Jaji Mkuu amewataka wahitimu wa Chuo hicho kuachana na fikira za kusubiria ajira katika sekta za Umma na binafsi badala yake wafikirie kujiajiri wenyewe katika sekta nyingine ambazo pengine hazitakuwa na uhusiano na kozi ya Sheria ambayo wameisomea.

Alisema hatua hiyo itawasaidia katika kukabiliana na ukosefu wa ajira na hvyo kujipatia kipato kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla huku akisisitiza kusema elimu ya sheria haimzuii mtu kufanya kazi aina nyingine.

"Digrii ya sheria haimzuii mtu kufanya kazi nyingine, tuanze kujitayarisha kisaikolojia kufanya kazi nyingine zile kazi tulizozizoea hazipo tena" alisema Jaji Mkuu huku akiwasihi Wahitimu hao kujitahidi kuwa kwenye Dunia inayoendana na yeknolojia.

Jaji Mkuu aliwataka Wahadhiri, Wanafunzi na watumishi wote katika Chuo hicho cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kujitahidi kupitia programu maalum za mafunzo ili kupata ujuzi, umahiri wa kutoa huduma katika mazingira ya kidijitali.

Alisema kikosi Kazi cha Mahakama kilichosimamiwa na Chuo hicho kilikamilisha Rasimu ya Mtaala wa kuendeshea mafunzo endelevu kwa watumishi wote wa Mahakama (BASIC DIGITAL SKILLS CURRICULUM FOR JUDICIARY STAFF).

Prof. Juma alisema ili mafunzo ya Mtaala huo kufanikiwa kwa watumishi wote wa Mahakama, Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kinatakiwa kuwa na uwezo wa kutoa mafunzo hayo ambayo yatatolewa na Chuo husika kwa njia ya kidijitali.

vilevile Jaji Mkuu wa Tanzania ameushukuru uongozi wa Wilaya na Wananchi Lushoto kwa kutoa eneo ukubwa mita za mraba (square mita) 8,000 kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Kisasa ya Wilaya hiyo.

Alisema uongozi wa Mahakama ya Tanzania utafanyika kazi eneo hilo ili jengo litakalojengwa liwe Mahakama ya Wilaya na litumike kutoka mafunzo kwa Vitendo kwa wanachuo wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama cha Lushoto.

Awalia Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzana Dkt. Paul Kihwelo alisema wamekamilisha uandaaji na uchapishaji wa kitabu kinachoelezea maisha ya Jaji wa Mahakama ya Rufaa Robert Habesh Kisanga kinachoitwa A Dream Coming to Fruition: A Biography of Justice Robert Habesh Kisanga ambacho uzinduzi wake utafanyika hivi karibuni.

Aidha Mkuu wa Chuo hicho alisema katika uboreshaji ufundishaji kwa wanachuo wameandaa Jukwa ya kufundishia kwa njia ya Kieletroniki ambapo wako katika hatua za mwisho na sasa taratibu zinaendelea kuwajengea uwezo Wataalamu wa namna ya kufundisha na kuandaa machapisho kwa njia ya mtandao.

Wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania Dkt. Gerald Ndika alisema kuwa Chuo hicho kimepata mafanikio makubwa katika utoaji wa Astashahada, Stashahada katika Sheria , uandaaji wa machapisho na uendeshaji wa warsha.

Alitanabaisha kuwa Chuo kimejikita katika ufafiti ambao umesaidia kukidhi matakwa ya wananchi huku kikiwa kimejika katika kutoa elimu inaendana na mabadiliko ya wakati na hivyo kuweza kumudu hali ya ushindani.

Post a Comment

0 Comments