Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR YAAHIDI KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA MICHEZO NCHI NZIMA.

20 Novemba, 2023

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa ahadi hiyo Ikulu, Zanzibar alipojumuika kwenye chakula cha mchana na wachezaji wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 15, Karume Boys, baada ya kunyakua kombe la CECAFA nchini Uganda.

Dk. Mwinyi alisema michezo ni afya, ajira, utalii pia huwaunganisha jamii kwa watu kufurahi pamoja na kuwa kitu kimoja.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema Zanzibar haitegemei utalii wa urithi pekee unaotokana na hifadhi ya Mji Mkongwe pamoja na fukwe lakini pia michezo ni utalii mkubwa na wakutegemewa.

Alisema Zanzibar inatarajiwa kuwa mwenyeji wa michuano ya AFCON mwaka 2027 hivyo imejipanga kuimarisha miundombinu ya kisasa kwenye sekta ya michezo pamoja na kushajihisha sekta ya utalii hususani hoteli na nyumba za kufikia wageni.

Naye Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita alisema Wizara ilipewa dhamana na Serikali ya kuisafirisha timu hiyo ambapo Rais Dk. Mwinyi alitoa usafiri wa ndege kwa Karume Boys kama zawadi wakati wa kurejea nchini.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Muhamed Said Dimwa alishauri kupatiwa mafunzo maalumu ya michezo walimu wawili kwa Karume Boys.

Kwa upande wake Rais wa ZFA, Suleiman Mahmoud Jabir alisema mafanikio ya ushindi wa Karume Boys yaliyokana na juhudi na ushirikiano wa wadau wengi nchini.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
Karume Boys Mabingwa wa Kombe la CECAFA U-15 kwa mwaka 2023-2024 wakiwa na Kombe lao la Ubingwa na Viongozi wa ZFF (kushoto ) Rais wa ZFF Suleiman Mahamoud Jabir wakiwa katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar, wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwasili katika viwanja hivyo kwa ajili ya kujumuika na Wachezaji katika chakula maalum alichowaandalia leo 20-11-2023.(Picha na Ikulu)
VIONGOZI wa Serikali wakiwa katika Viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar wakihudhuria dhifa maalum iliyoandaliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi kwa ajili ya kuwapongeza Wachezaji wa Timu ya Karume Boys U-15 iliyotowa Ubingwa wa CECAFA U-15 katika mchezo wa Fainali na Timu ya Taifa ya Uganda U-15 uliofanyika wiki iliyopita Nchini Uganda kwa ushindi wa bao 4-3 (Picha na Ikulu)
WACHEZAJI wa Timu ya Karume Boys U-15 wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwapongeza kwa kuchukua Ubingwa wa Kombe la CECAFA U-15, katika mchezo wa fainali na Timu ya Uganda uliyofanyika Nchini Uganda wiki iliyopita, wakati wa dhifa maalum ya chakula na kuwapongeza iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar leo 20-11-2023.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza wakati wa Dhifa Maalum ya chakula maalum alichowaandaliwa Wachezaji wa Timu ya Karume Boys U-15 kwa ushindi wa Ubingwa wa Kombe la CECAFA U-15 kwa kuifunga Timu ya Taifa ya Uganda u-15 katika mchezo wa Fainali uliofanyika Nchini Uganda wiki iliyopita, hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar leo 20-11-2023.(Picha na Ikulu)

Post a Comment

0 Comments