Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU MAJALIWA MGENI RASMI KONGAMANO LA FURSA MKOANI TANGA


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

KONGAMANO kubwa la kuangalia fursa za uwekezaji Mkoa wa Tanga linatarajiwa kufanyika kesho Novemba 16 na 17 katika ukumbi wa Hoteli ya Legal Naivera jijini humo.

Akiongea ofisini kwake, mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amesema kongamano hilo la pekee ambalo liliwahi kufanyika miaka kumi iliyopita mkoani humo, litawashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo wa ndani na nje ya Mkoa huo.


"Kwahiyo ni muhimu sana wale wote ambao tumewakaribisha na waliopanga kuja wahakikishe kesho wanawahi ifikapo saa mbili asubuhi, katika tukio hilo mgeni rasmi tunategemea atakuwepo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,


"Ni tukio kubwa sana na la kihistoria katika Mkoa wa Tanga, kwa sababu tukio la namna hii lilifanyika miaka kumi iliyopita wakati huo mkuu wa Mkoa alikuwa mama Chiku Galawa, lakini linajitokeza tena mwaka huu ikiwa mambo mengi mazuri ya maendeleo yameshafanyika" amesema.


Kindamba amefafanua kuhusu maendeleo hayo mojawapo ikiwa ni bandari ya Tanga kuboreshwa na kuimarishwa ambapo serikali ya awamu ya sita imewekeza zaidi ya sh bilioni 429 na kuifanya kuwa moja kati ya bandari kubwa na kwasasa meli kubwa zimeanza kushuka Tanga.


Pia amebainisha kwamba maboresho mengine yameendelea kufanyika hasa katika zao la mkonge kwakuwa zao hilo ndilo lililokuwa likibeba uchumi wa nchi.


"Lakini pia kuna ujenzi mkubwa wa bomba la mafuta kutoka nchini Uganda ambao umegarimu zaidi ya dola bilioni 5, ni uchumi mkubwa kwahiyo Tanga tumejipanga na tumejiandaa kuushikilia,


"Jingine ambalo tupo nalo ni uendelezaji wa miundombinu ya kimkakati ambavyo ni mashua na maboti yanayokuja yakiunganisha visiwa wa Zanzibar na Tanga na tunatarajia miezi michache ijayo tutapokea meli ya mizigo, kwahiyo Tanga imefunguka na itaendelea kufunguka" amebainisha.


Mbali na hayo, Kindama amesema uwanja wa ndege mkoani humo unaendelea kuboreshwa ikiwa ni pamoja na barabara ya Tanga - Pangani - Saadani hadi Bagamoyo ambayo serikali imepanga kukamilisha kabla haujafika uchaguzi mkuu mwaka 2025.


"Katika kipande hicho cha km 50, Mh. Rais amejenga daraja lenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 83, tuwakaribishe wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi, na ndiyo maana kongamano letu tutakuwa na mabalozi wa nje ambao wataruhusiwa kuuliza maswali yao" amesisitiza.

Post a Comment

0 Comments