Ticker

6/recent/ticker-posts

CHUO KIKUU MZUMBE KULETA MABADILIKO MAKUBWA KATIKA SHUGHULI ZA UTAFITI

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Profesa William Mwegoha amewataka wanataaluma wanaoshiriki warsha ya uandaaji wa maandiko ya Miradi ya utafiti kuibua mawazo ya miradi mikubwa ya utafiti kwakuwa Chuo Kikuu Mzumbe kinafanya mageuzi makubwa katika eneo la tafiti.

Profesa Mwegoha ameyasema hayo tarehe 23 Januari 2024 alipokuwa akifunga warsha ya siku mbili kuhusu uandishi wa miradi mikubwa ya tafiti kwa wanataaluma wa Chuo Kikuu Mzumbe.

Warsha hiyo imendaliwa na Skuli ya Biashara ya Chuo Kikuu Mzumbe kupitia mradi wa "Crowdfunding for Youth Entrepreneurship in Tanzania (C4YET)"kwa kushirikiana na Kurugezi ya Tafiti, Machapisho na Mafunzo ya Shahada za Uzamili iliyofanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Maendeleo USA River, Arusha.

Amesema wanataaluma wakifanikiwa kuandaa na kuwasilisha mapendekezo ya miradi ya utafiti yenye ubora na sifa za kupata ufadhili wa kifedha watakiwezesha Chuo kupata fedha kupitia tafiti, bali pia itaongeza fursa kwa wanataaluma kujengewa uwezo kupitia masomo katika ngazi ya Umahiri na Uzamili.

Aidha, Profesa Mwegoha amesema kuwa chuo hakiwezi kuwa na maendeleo makubwa kama hakitakuwa na miradi mikubwa ya utafiti na kuongeza kwamba kwa sasa hivi chuo kina miradi inayoendelea lakini mingi kati ya hiyo inakaribia kumalizika. Hivyo, Menejimenti ya chuo imeweka jitihada za makusudi za kuwajengea wataalamu uwezo wa kuandika miradi na warsha hii ni sehemu mojawapo ya jitihada hizo.

“Asilimia 60 ya wafanyakazi wa chuo ni vijana, na chuo kina jukumu la kuwajengea uwezo katika eneo la tafiti. Kwa kutumia nguvu kazi hii ya vijana, chuo kinaweza kujenga ushirikiano wa ndani miongoni mwa wanataaluma lakini pia na vyuo vingine hapa nchini na vyuo vingine vya nje ya nchi, jambo ambalo ni muhimu. Alisisitiza Profesa Mwegoha.

Prof. Mwegoha aliongeza kuwa Menejimenti ya Chuo itaendelea kuunga mkono juhudi hizo na kuhakikisha kwamba zinazaa matunda ili Chuo kiweze kupata miradi mingi ambayo pia itatengeneza machapisho ya kutosha ambayo yatapandisha kiwango cha sifa ya Chuo kitaifa na kimataifa katika medani za kitaaluma.

Akihitimisha Mafunzo hayo Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha amesisitiza washiriki wa Warsha hiyo kuendeleza mawazo na maono yao katika miradi wanayoiandika na kuwataka kufanya jukumu hilo kwa bidii na weledi wa hali ya juu.

Kwa upande wake, mwezeshaji wa Warsha hiyo, Prof. Enno Hofeldt kutoka Denmark, amesema kuwa ili kuandaa pendekezo la mradi wa utafiti wenye sifa za ushindani kimataifa lazima kuzingatia dira ya nchi na ya dunia wakati wa kuandaa mapendekezo ya utafiti. Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kutambua masharti ya wafadhili wa miradi hii, kiasi cha fedha wanachoweza kufadhili, na aina ya tafiti wanazozifadhili.

Awali akitoa akitoa maelezo wakati wa warsha hiyo, Mratibu wa Mradi wa C4YET na Mhadhiri mwandamizi wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Nsubili Isaga, amebainisha kuwa mradi wa "Crowdfunding for Youth Entrepreneurs in Tanzania (C4YET)" chuo kikuu Mzumbe umelenga kuimarisha uwezo wa wanataaluma katika kuandaa na kuwasilisha mapendekezo ya miradi ya utafiti yenye uwezo wa kupata fedha na kusaidia jamii kushughulikia changamoto za kiuchumi.

Kwa upande mwingine Mkurugenzi wa tafiti, machapisho na Mafunzo ya uzamili Prof. Haruni Mapesa amemshukuru Profesa Enno kwa mafunzo aliyoyatoa maana yataleta uhakika wa maandiko ya miradi yenye matokeo makubwa na yenye kuleta manufaa kwa jamii ana wataaluma wataweza kuandika miradi ya kimataifa ambayo inafadhiliwa na mashirika makubwa ya kimataifa kama Danida Fellowship Center.

Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii Dkt. Halord Utouh akiongea kwa niaba ya wanataaluma amesema mafunzo yamewazesha wanataaluma kupata uwezo wa kuandaa miradi kwani kazi kubwa ya chuo chochote ni kutoa mafunzo, kufanya tatiti na kutoa ushauri wa kitaalamu.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Mzumbe Prof. William Mwegoha akizungumza wakati wa Kufunga warsha ya kuandaa Miradi ya Utafiti kwa wanataaluma wa Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Mradi wa C4YET.
Mshauri Mkuu wa Masuala ya Utafiti, Prof. Enno Hofeldt kutoka Shule ya Biashara ya Copenhagen (Denmark), akifafanua kwa ufupi mbele ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Mzumbe Prof. William Mwegoha yale aliyoyafundisha kwa wanataaluma wa Chuo Kikuu Mzumbe kuhusiana na namna ya kuandaa mapendekezo ya Utafiti  kupitia Mradi wa C4YET.
Mtiva wa Kitivo cha Sayansi za Jamii, Mhadhiri Mwandamizi Dkt. Harold Utouh kutoka  Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wanataaluma kutoka  Chuo Kikuu Mzumbe waliohudhuria warsha ya kuandaa Miradi ya Utafiti kupitia Mradi wa C4YET mbele ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Mzumbe Prof. William Mwegoha.
Mkurugenzi wa Tafiti, Machapisho na masomo ya Uzamili Prof. Haruni Mapesa akitoa utambulisho wa wanataaluma wote waliohudhuria warsha ya kujifunza kuandaa na kuwasilisha mapendekezo ya Miradi ya Utafiti yenye uwezo wa kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii kupitia Mradi wa C4YET.
Mhadhiri Msaidizi Chuo Kikuu Mzumbe na Mratibu wa ujasiriamali na Mahusiano ya Viwanda Dkt. Felister Tibamanya akieleza namna yeye na wanataaluma wenzake walivyojidhatiti kufanyia kazi yale waliyojifunza katika warsha ya uandaaji wa Miradi ya Utafiti kwa wanataaluma wa Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Mradi wa C4YET.

Post a Comment

0 Comments