Ticker

6/recent/ticker-posts

WAJUMBE WAMTAKA MBUNGE WAO ASIELEZEE SANA KAZI ALIZOFANYA KWANI WAO WATASEMA.

Na Mwandishi wetu;-

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Butiama wamemuomba Mbunge wa Jimbo la Butiama na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini kwamba asihangaike kuelezea sana miradi ya kimaendeleo iliyotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kwani wao ndio kazi yao ya kuyaelezea.

Hayo yameibuka kwenye Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Butiama uliofanyika Januari 26, 2024 katika Viwanja vya Mwenge Butiama, wakati Mbunge wa Jimbo hilo akisoma taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa Kipindi cha Miaka yake mitatu na wajumbe wakaanza kupiga kelele sauti tofauti tofauti zikimtaka asielelezee sana miradi ya kimaendeleo kwani wao sio vipofu wanaona kazi nzuri iliyofanyika.

"Acha kusumbuka Mhe. Mbunge tulichokutuma tumekiona na tumejilidhisha sisi sio vipofu tuna imani na wewe Mungu akupe maisha marefu ufanye mengi zaidi" alisikika Mjumbe kutoka Kata ya Bukabwa.

Huku wengine wakisikika "Wewe chapa kazi kwani mara kwa mara tumekuwa tukikuona hapa jimboni unatuletea miradi mingi na muda mwingi unapatikana jimboni ingawa ni Naibu Waziri"

Katika Mkutano huo Mgeni Rasmi alikuwa Katibu wa NEC Oganaizesheni CCM Taifa Ndg. Issa Haji Ussi Gavu kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Ndg. Abdulrahman Kinana.

Hata hivyo, awali Mbunge huyo alielezea baadhi ya miradi iliyofanyika kwa kipindi chake ambayo ni Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia, Hospitali ya Wilaya, Barabara ya Makutano Sanzante, Chuo cha VETA, Shule za Sekondari nane mpya, lambo la Bukabwa, kutoka vituo viwili vya afya hadi vitano, zahanati kutoka 16 hadi 32, Ujenzi wa kituo cha Polisi, Ofisi ya Uhamiaji, Ofisi za Halmashauri, nyumba za Katibu Tawala na Mkurugenzi, Ofisi ya mdhibiti ubora nk.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mara Ndg. Patrick Chandi, Katibu wa CCM Mkoa, Mwenyekiti wa UWT CCM Mkoa wa Mara Bi. Nancy Msafiri, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mtanda na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji walishiriki ambapo kila mmoja wao alitoa shuhuda yake.

Wengine ni Mjumbe wa Halmshauri Kuu CCM Taifa Ndg. Joyce Mang'o, Mjumbe wa Baraza Kuu UWT CCM Taifa Ndg. Mariam Sagini, Mjumbe wa UWT CCM Taifa Mkoa wa Mara Rhobi Samwelly na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Mara Ndg. Julius Masubo.

Aidha, Mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe wa kamati ya siasa mkoa, wenyeviti wa CCM Wilaya ya Musoma, Bunda, Tarime pia Wenyeviti wa Halmashauri na viongozi wa dini.

Post a Comment

0 Comments