Ticker

6/recent/ticker-posts

ENG. SANGA AWAFUNDA WATUMISHI WA ARDHI NCHINI

--Awataka kuwa wasuluhishi wa migogoro na sio chanzo

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amewaasa watumishi wa Sekta ya Ardhi kote Nchini kujiepusha na tabia ya kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi na badala yake wawe wafumbuzi wa migogoro.

Ametoa rai hiyo Februari 9, 2024 Mkoani Tabora wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji wa Sekta ya Ardhi pamoja na kuzungumza na watumishi Mkoani Tabora.

"Serikali imewapa dhamana ya kuwahudumia wananchi katika masuala ya ardhi; mnapaswa kusaidia kusuluhisha migogoro na sio kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi," amesisitiza

Katibu Mkuu Sanga. Mhandisi Sanga amesema anatambua uwepo wa watumishi ambao ni waadilifu hata hivyo wapo wachache ambao wamekuwa wakisababisha uwepo wa migogoro.

Amewasisitiza kufanya kazi kwa uadilifu na weledi katika kutimiza majukumu yao bila kusahau kuzingatia Sheria, Taratibu, Kanuni na Miongozo iliyopo.

"Sisi viongozi wenu hatuko tayari kuona mtumishi anakua chanzo cha mgogoro wa ardhi na hatua stahiki zitaendelea kuchukuliwa kwa watumishi watakaobainika kusumbua wananchi," amesisitiza Mhandisi Sanga.

Amesema Sekta ya Ardhi inayo miongozo yake na hivyo kila mtumishi anapaswa kuhakikisha anatimiza wajibu wake kwa kufuata miongozo husika ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanapatiwa ufumbuzi wa kero wanazowasilisha.

"Ninawasihi kuhakikisha mnatoa majawabu ya uhakika kwa wananchi badala ya kuwapiga danadana na kuwazungusha bila sababu. Mwananchi ajisikie kuwa kuhudumiwa vizuri katika sekta ya ardhi siyo anasa bali ni haki yake," amesisitiza Mhandisi Sanga.

Aidha, amewataka watumishi Sekta ya Ardhi kote Nchini kujenga tabia ya kuonyana wenyewe kwa wenyewe pindi mmoja wao anapokwenda kinyume na kanuni za utumishi wa umma.

Amebainisha kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejizatiti kuimarisha huduma kwa wananchi wake na kwa kuboresha utendaji ikiwa ni pamoja na kununua magari mawili kwa kila Mkoa sambamba na ujenzi wa Ofisi za Ardhi za Mikoa kwa Mikoa 25 Tanzania Bara.

Akizungumzia suala la kodi ya ardhi, Mhandisi Sanga amesisitiza suala la ukusanyaji mapato kupitia kodi ya pango la ardhi na amewataka Makamishna wa Ardhi Wasaidizi kote nchini kulisimamia jambo hilo kikamilifu kwa kuweka mikakati madhubuti.

Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Sanga amekagua miradi inayotekelezwa na Chuo Cha ardhi Tabora (ARITA) pamoja na kujadili changamoto zinazokikabili chuo hicho.

Akiwa chuoni hapo, Mhandisi Sanga ameeleleza uongozi wa chuo kukaa na kutafakari namna bora ya kuwa na mipango thabiti ya kuboresha mitaala na miundombinu ya chuo ili kiweze kujiendesha katika hali ya ushindani na vyuo vingine. Amebainisha kuwa timu ndogo itaundwa mahsusi kwa ajili ya kuandaa mapendekezo ya namna bora ya kuboresha utendaji wa chuo.

Post a Comment

0 Comments