Ticker

6/recent/ticker-posts

MTATURU:SERIKALI IWEZESHENI TPA IFANYE KAZI KWA UFANISI

Mbunge wa Singida Mashariki Mhe.Miraji Mtaturu,akichangia taarifa ya utendaji ya Kamati ya Bunge ya Miundombimu Kuhusu shughuli zake kwa Mwaka 2023 bungeni Dodoma.

Na.Mwandishi Wetu-DODOMA

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amechangia taarifa ya kazi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kipindi cha mwaka 2023,huku akiishauri serikali mambo matatu ikiwemo kuboresha miundombinu ya bandari nchini.

Akichangia taarifa hiyo Februari 5,2024,Bungeni Jijini Dodoma,Mtaturu amesema ni lazima serikali ione namna ya kuongeza fedha kwa ajili ya kuiboresha na kuisaidia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),ili iongeze ufanisi wake.

Amesema kwenye taarifa iliyosomwa na Mwenyekiti wa kamati ya Miundombinu,wamegundua baadhi ya mambo mbalimbali ambayo yanakwamisha suala la usafirishaji wa mizigo ikiwemo foleni kubwa ya meli katika bandari hiyo.

Ameeleza kuwa pamoja na juhudi zote bado kuna tatizo kubwa la ushushaji wa mizigo kwa wakati hivyo jitihada mbalimbali zinapaswa zichukuliwe.

“Kwanza lazima tukubali kwamba Bandari ya Dar es salaam imekuwa kivutio kikubwa cha ukanda wa nchi nane ndio maana kunakuja wateja wengi katika kipindi hiki,lakini kipindi cha Disemba kuanzia Novemba mpaka Januari kumekuwa na mizigo mingi inapokelewa kwa sababu ya msimu,

“Katika msimu wa kilimo nchi yetu imekuwa inahamasisha wakulima kutumia mbolea lakini pili mbegu bora tumekuwa tukizitumia maana yake zinatoka nje ya nchi kwa hiyo hapa nchini zinakuja kwa njia ya meli ,kwa hiyo kuona meli nyingi pia ni mafanikio kwa kuwa watu wameona destination ya Dar ni nzuri kushushia mizigo yao,haya ni mafanikio makubwa sasa lazima yazae changamoto,”amesema.

Mtaturu amesema kamati ilivyowahoji TPA walisema wanatakiwa waongeze gati 12 mpaka 15 ili kuongeza uwezo wa ushushaji wa meli nyingi kwa wakati mmoja kwa hiyo kazi hiyo inahitaji uwekezaji.

“Kama ambavyo wote tunajua TPA kwa maana ya bandari ndio lango kuu la uchumi,tumekuwa tukitegemea fedha nyingi kukusanya kupitia bandari yetu,katika kipindi cha taarifa tumejulishwa kwamba tumeweza kuhudumia nyongeza 5 kwa maana asilimia 17.5 kuacha ya mwaka uliopita,tumeweza kuhudumia kutoka tani milioni 5.81 kwenda tani mil 6.85 maana yake pamoja na yote kuna hatua kubwa tumepiga katika kuhudumia shehena kwenye bandari yetu ya Dar,

“Mbali na hayo mapato yameongezeka kutoka Sh Bilioni 310.78 hadi Sh Bilioni 365.12 katika hiki kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2023/2024,pamoja na juhudi zote hizi na kwa sababu asilimia 90 ya mzigo wote unaosafirishwa unatoka kwenye bandari ya Dar maana yake Bandari ya Dar es salaam ikiboreshwa itakuwa na uwezo mkubwa wa kuingiza mapato ya serikali,”amesema.

Amesema maboresho yakifanyika yataongeza kasi ya ushushaji wa mafuta lakini pia utapunguza gharama ya mafuta nchini katika soko la kawaida.

“Kama alivyosema mwenzangu aliyetangulia kwamba kama unataka kumkamua ng’ombe lazima umlishe chakula cha kutosha ambayo ni majani,kwa hiyo kwenye hili kuna suala pia la ushushaji wa mafuta katika gati ile ya mafuta ya KLJ, eneo lile ni dogo meli za mafuta pia zimekuwa zikisubiri kwa hiyo utatuzi wake ni kwamba lazima ujenge eneo lingine la kuhifadhia mafuta ambayo ni single receiving terminal ambayo wanaita SRT,

“Ukijenga hii SRT utaweza kufanya storage wakati unasubiri wateja ambao wameagiza mafuta hayo kuyapokea na pia itapunguza gharama ya mafuta nchini katika soko la kawaida,”ameongeza.

Amesema ili kuwa na ushindani na bandari nyingine ni lazima TPA wawe na pesa .

“Kama haitoshi tumeona kwamba waferji hii ambayo inatajwa huko nyuma ilikuwa TPA wanaachiwa na serikali,hii ni kama vile kufanya parking ya meli katika eneo la bandari wala haihusiani na mapato ya TRA, huko nyuma walikuwa wanafanya wenyewe wanazikusanya hizi pesa na wanafanya miradi mbalimbali ya ndani kwa hiyo maana yake serikali inapochukua hela yote inapeleka katika mfuko mkuu wa serikali,

“Hii inaifanya TPA ishindwe hata kununua chochote mpaka iombe kwanza hazina kwa hiyo niombe sana kama ilivyosemwa kwenye taarifa waferji irudi waachiwe TPA waweze kukusanya na wakikusanya watakuwa na uwezo wa kuendeleza miundombinu ya bandari na kuvutia zaidi ushushaji wa mizigo lakini kama haitoshi tuwaachie asilimia 30 ambayo itabaki kwenye bandari ili isaidie,”amesema.

Ametaja jambo la pili kuwa ni suala la ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), itakuwa ni sapoti kubwa ya kuondoa mizigo bandarini lakini SGR haijakamilika kwa muda mrefu.

“Niombe kwamba SGR ikikamilika watakuwa na uwezo wa kutoa Tani zaidi ya Milioni 17 kwa wakati mmoja kwa hiyo watapunguza msongamano wa Dar es salaam,lakini pia itasaidia kulinda barabara zetu zisiharibike,niombe sana kama inawezekana wenzetu wa SGR waharakishe,”ameongeza.

Jambo la tatu alilolishauri Mtaturu ni suala la Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS),ambao wamekuwa wakisaidia sana na serikali imekuwa inategemea miundombinu ili iweze kupeleka huduma nchini hivyo kama miundombinu sio imara hakuna kitakachofanyika,watu hawatasafiri na uchumi hautaenda mbele.

“Ombi langu kwa serikali naomba tujitahidi sana wenzetu wa TANROADS waongezewe fedha wanazoziomba ambazo zitasaidia kwenda kuboresha barabara, lakini barabara zilizopitishwa na bunge zimesainiwa kupitia mradi ule au utaratibu wa EPC+ F zenye urefu wa kilomita 2,035 mpaka leo hakuna iliyoanza kufanya kazi,

“Mbali na kutoanza kufanya kazi,pia haijaanza kujengwa na tumebakiza miezi sita ya bajeti hii kukamilika,wenzetu wanahitaji fedha zaidi ya Trilioni 3.75 bila VAT ili waweze kuanza miradi hii,miradi hii ni pamoja na barabara ya urefu wa kilomita 460 kutoka Singida Kwa Mtoro kwenda mpaka kule Tanga,barabara hii ni miongoni mwa barabara saba zilizopitishwa katika kujenga,niombe serikali kwa sababu miundombinu ni uchumi iweke jicho katika kuhakikisha barabara inakamilika,”ameomba.

Mbali na maombi hayo amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha nyingi katika taasisi ambazo leo zimetoa huduma mbalimbali kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments