Ticker

6/recent/ticker-posts

WALIOFARIKI KWENYE AJALI ARUSHA WAFIKA 25



Watu 25 wamefariki dunia huku wengine ishirini na moja (21) wakijeruhiwa katika ajali iliyotokea maeneo ya Ngaramtoni kibaoni by Pass ikihusisha Lori na magari mengine madogo matatu Wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha.

Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi CP Awadhi Juma Haji akiwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru amesema ajali hiyo ilitokea Februari 24,2024 muda wa saa 11:00 jioni katika Barabara ya Arusha Namanga 

Ajali hiyo ilihusisha lori lenye namba za usajili KAC 943 H aina ya Mack lenye tela namba za usajili ZF 6778 mali ya kampuni ya KAY Construction ya Nairobi Nchini Kenya.

CP Awadhi ametaja idadi ya waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni wanaume (14) wanawake (10) na mtoto mmoja wa kike ambao jumla yao ni (25) huku akiitaja idadi ya raia wa kigeni waliofariki kuwa ni saba (07).

Katika ajali hiyo pia CP Awadhi ametaja idadi ya majeruhi kuwa ni 21 kati yao wanaume ni kumi na nne (14) na wanawake ni saba (07)

Imeelezwa kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kufeli breki ya lori kitendo kilichopelekea lori hilo kuyagonga magari mengine yalikuwa mbele yake ambapo Jeshi la polisi linaendelea kumtafuta dereva aliyesababisha ajali hiyo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake. 

Chanzo cha habari -EastAfricaTV

Post a Comment

0 Comments