Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKAMU ATAKA CHUO CHA VETA WILAYA YA MKINGA KUANZISHWA UFUGAJI SAMAKI.



****************


Na Hamida Kamchalla, MKINGA.


MAKAMU wa Rais, Dkt. Philip Mpango ameagiza uanzishwaji wa ufugaji wa samaki katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika Wilaya ya Mkinga, lakini pia mazingira mazuri ili kupata wataalamu wengi kutoka chuoni humo.


Makamu ameyasema hayo alipofanya ziara yake ya kikazi ambapo alizindua na kuweka jiwe la msingi ikiwa ni pamoja na kupanda mti wa kumbukumbu katika chuo hicho.


"Muhakikishe kwamba chuo hiki kinawezeshwa uanzishwaji wa ufugaji wa samaki mara moja, ndugu zangu maelekezo ninayoyatoa ningeomba sana myazingatie na kuyatekeleza" amesema.


Aidha amewataka wananchi wilayani humo kujitahidi kupanda miti katika kaya zao na kuweka hali nzuri ya utunzaji wa mazingira ili kuepuka majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi yanayotokea.


"Ndugu zangu, nchi yetu sasa hali siyo nzuri, kwahiyo nawaombeni sana Wanamkinga, kila mtu akapande walau miti mitatu tu katika kaya yake, tukapande miti ya matunda watoto wetu waendelee kufaidi, lakini pia miti ya kivuli ili mkapendezeshe maeneo yetu,


"Hii ndiyo itasaidia kuondoa adha ambayo tumeanza kuipata katika Taifa letu, mvua hazitabiriki zikija ni nyingi sana kupitiliza, barabara zinaharibika, magonjwa yanaongezeka kwa sababu hatutunzi mazingira yetu, hivyo nataka niwasihi sana tuweze kutunza na kuendeleza mazingira yetu" amefafanua.


Amebainisha kwamba muhimu pia kuhakikisha mazingira ya chuo hicho yanakuwa bora zaidi ili kuweza kuwafanya wanafunzi kuwa na utaratibu wa kujifunza kulinda na kutunza mazingira katika maeneo yao hata watakapokuwa wamehitimu.


"Kwahiyo niwaombe wananchi, taasisi binafsi, taasisi za kidini na wadau wengine kushirikiana na serikali kutengeneza wataalamu wengi zaidi kwenye fans mbalimbali, lakini hasa katika masomo ya sayansi, ubunifu, tekinolojia na ufundi" amesisitiza.


Naye mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Tanga, Mwanaisha Ulenge amesema uwepo wa chuo hicho wilayani humo utasaidia vijana kujikwamua kiuchumi na maendeleo kuweza kupatikana.


Ulenge pia ameiomba serikali kuweza kufanya ukarabati wa jengo la maktaba la Mkoa wa Tanga kutokana na uchakavu uliopo kutokana na kujengwa miaka mingi iliyopita kabla ya uhuru wa nchi.


"Naomba niseme kwamba tunaishukuru serikali kwa maendeleo makubwa inayotupatia, lakini niikumbushe jambo moja la kielimu ambalo limesahaulika katika Mkoa huu,


"Maktaba ya Mkoa imeanzishwa mwaka 1558, ni kongwe kuliko uhuru wa nchi hii, naomba sana maktaba ile ifanywe iwe ya kisasa kwa sababu ukiingia ndani ya jengo lile ni chakavu kuliko maelezo, lakinibpoa haina vitabu, hivyo tunaomba tuongezewe na vitabu" amesema Ulenge.

Post a Comment

0 Comments